July 4, 2016

MCHEZAJI WA ASILI YA DR CONGO AJIUNGA NA CHELSEAKlabu ya Chelsea ya Uingereza imemsajili mshambuliaji wa Ubelgiji mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Michy Batshuayi amehamia Chelsea kutoka klabu ya Marseille ya Ufaransa na kutia saini mkataba wa miaka mitano. Mamake ni Viviane Leya Iseka na babake Pino Batshuayi.

Michy alikuwa na fursa ya kuchezea timu ya taifa ya DR Congo kutokana na asili ya wazazi wake lakini mwaka jana aliamua kuwa mchezaji wa Ubelgiji. Aliwachezea mechi ya kwanza dhidi ya Cyprus Machi 2015 na kufunga bao.

Michy, 22, ambaye ndiye mchezaji wa kwanza kununuliwa na meneja mpya wa Chelsea Antonio Conte Stamford Bridge, hujulikana kwa jina la utani kama Batsman. Kakake Aaron Leya Iseka ni mchezaji wa klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji. Chelsea hawakutangaza wazi bei waliyomnunua Michy lakini inaaminika kuwa takriban £33m (euro 40m).

Mshambuliaji huyo, aliyefunga mabao 23 akichezea Marseille msimu uliopita, alifungia Ubelgiji wakati wa ushindi wao hatua ya 16 bora dhidi ya Hungary katika Euro 2016 na pia aliwachezea walipotolewa kwenye michuano hiyo hatua ya robofainali na Wales.

"Nina furaha isiyo na kifani kujiunga na moja ya klabu kubwa Zaidi Ulaya,” alisema Batshuayi. "[Wachezaji wenzangu Ubelgiji] Eden Hazard na Thibaut Courtois wameniambia mambo mengi mema kuhusu klabu hii, na ikizingatiwa kwamba Antonio Conte anaingia, ni wakati mzuri sana kuwa mchezaji wa Chelsea."