June 11, 2016

TAARIFA YA KUKANUSHA TAARIFA ZINAZOENEZWA KWENYE VYOMBO VYA HABARI JUU YA KUSITISHA AJIRA ZA WALIMU


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Yah: KUKANUSHA TAARIFA ZINAZOENEZWA KWENYE VYOMBO VYA HABARI JUU YA KUSITISHA AJIRA ZA WALIMU KWA MWAKA 2015/2016

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa mbalimbali kwa vyombo vya habari na Umma zinazosambazwa katika mitandao ya Kijamii juu ya kusitishwa kwa ajira za Ualimu kwa mwaka 2015/2016.

Taarifa hizi zinaeleza kuwa kuna utafiti uliofanywa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI na kubaini kuwepo kwa ziada ya Walimu wa Sanaa na Biashara katika Shule za Msingi na Sekondari wapatao 7,988. Taarifa hizi zinadai kuwa Serikali imesitisha ajira za Walimu wa Sanaa na Biashara hadi hapo itakapokuwa na uhitaji huo, na kwamba Serikali inatarajia kuwaajiri Walimu wa Sayansi na Hisabati mnamo mwezi Novemba baada ya Walimu kutoka Vyuo mbalimbali nchini kumaliza masomo ili waweze kuajiriwa na waliomaliza mwaka 2015.

Taarifa hiyo inaonesha imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tarehe 10/06/2016. Ofisi ya Rais – TAMISEMI inapenda kuutaka Umma kupuuza taarifa hiyo na kutoiamini kwa kuwa haijaandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Ofisi ya Rais- TAMISEMI.

Ofisi ya Rais –TAMISEMI inapenda kujuulisha Umma kuwa taarifa hiyo ni batili na waipuuze kwani mpaka sasa Ofisi ya Rais-TAMISEMI haijatangaza ajira za walimu na endapo ajira hizo zitakuwa tayari zitatangazwa rasmi kwenye vyombo vya habari na kupitia tovuti ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI www.tamisemi.go.tz.

Ofisi ya Rais –TAMISEMI inawataka wale wote wanaoghushi taarifa na kuzitangaza kwenye vyombo vya haabari kwa kisingizio kuwa zimetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kuacha mara moja tabia hiyo kwani haitasita kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kujihusisha na kughushi taarifa na kuzisambaza kwenye vyombo vya habari.

Imetolew na
Kitengo cha Mawasilisho Serikalini,
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
10/06/2016