June 22, 2016

Serikali yapiga marufuku usambazaji wa sukari ya KK na kuiondoa sokoni mara mojaAkiongea na Waandishi wa Habari leo mjini Dodoma,Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Charles Mwijage,amepiga marufuku mara moja matumizi ya sukari aina ya Kijiko Kimoja (KK) bila ushauri wa daktari.
Sukari hiyo aina ya KK imeamuliwa kurudishwa Dsm toka katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Mwanza ambapo tayari ilishaanza kuuzwa.

Waziri Mwijage anasema sukari hiyo inapaswa kuuzwa kwenye maduka maalumu(Super markets) na Maduka ya dawa Maalumu(Pharmacy) kwa sababu matumizi yake yanahitaji ushauri wa daktari kwa mtumiaji.
Mwijage anasema madhara ya sukari hiyo ni pamoja na kuharibika kwa mimba changa kwa wanawake wajawazito na madhara mengine makubwa ya kiafya.

Sukari hiyo imeamuliwa kutolewa kwenye magodown yote eneo la kanda ya ziwa na mkoa wa Kigoma na kurudishwa Dsm.

Mamlaka husika kama TFDA,TRA,TBS,Wizara ya Afya na mamlaka za Wizara ya Viwanda na Biashara zimeamuliwa kuiondoa sokoni sukari hiyo haraka iwezekanavyo na msambazaji kuacha mara moja kusambaza sukari hiyo kwa wananchi kwani ina madhara makubwa.

Licha ya kuwa Taifa lina uhaba mkubwa wa sukari,lakini serikali haipo tayari kuangamiza afya za watu wake kwa kuruhusu sukari isiyo "rafiki" kwa afya na maisha ya watu.Sukari ya KK inasemwa kuwa na utamu usio wa kawaida,kijiko kimoja tu cha sukari kinaunga kikombe cha ujazo wa lita moja ambayo ni hatari kwa afya.