May 31, 2016

WABUNGE WA UPINZANI WASIMAMISHWA KUHUDHURIA VIKAO VYA BUNGE
TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU UCHUNGUZI WA VITENDO VYA BAADHI YA WABUNGE KUFANYA VURUGU BUNGENI NA KUDHARAU MAMLAKA YA SPIKA TAREHE 27 JANUARI, 2016


UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 4 fasili (2) na (3) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 naomba kuwasilisha Mbele ya Bunge lako Tukufu Taarifa ya Kamati baadhi ya Wabunge kufanya vurugu Bungeni na kudharau Mamlaka ya Spika siku ya tarehe 27 Januari, 2016 katika Mkutano wa Pili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kukushukuru wewe binafsi kwa weledi, busara na hekima unazozitumia katika kuliongoza Bunge letu kwa ufanisi mkubwa. Kama tujuavyo Bunge la Kumi na Moja lina changamoto nyingi kutokana na ukweli kwamba, karibu asilimia sabini ya Wabunge wa Bunge letu inaundwa na Wabunge wapya kabisa kwa maana ya uzoefu wa masuala ya kibunge na pia kuwepo kwa wabunge wengi ambao ni vijana.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kumshukuru Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujasiri na umahiri alionao katika kumsaidia Spika kuliongoza Bunge letu.

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 31 Januari, 2016 kwa mamlaka uliyonayo chini ya Fasili ya 4(1) (a) na (b) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016, uliiagiza Kamati yangu kushughulikia suala la vitendo vya baadhi ya wabunge waliodaiwa kufanya vurugu Bungeni na kudharau Mamlaka ya Spika siku ya tarehe 27 Januari, 2016. Katika maelekezo hayo, uliitaka Kamati yangu kufanya uchunguzi ili kubaini kama wabunge wafuatao walihusika katika kufanya vurugu Bungeni katika tarehe tajwa.

(i) Mhe.Tundu A. Lissu, (Mb);

Mhe.Godbless J. Lema, (Mb);

Mhe.Pauline Gekul, (Mb);na

Mhe.Ester A. Bulaya, (Mb).

Mheshimiwa Spika, baada ya maelekezo hayo, Ofisi ya Bunge iliandaa Hati ya Wito (Summons) na kumkabidhi kila Shahidi (Mbunge) ili afike mbele ya Kamati kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mheshimiwa Spika, hati hiyo ya Wito ilimtaka kila shahidi kutoa maelezo, kwanini asichukuliwe hatua kwa kukiuka Kanuni zifuatazo; Kanuni ya 72(1), 68(10), 60(2), 74(1) (a) na (b) ambazo zinakataza Wabunge kufanya kitendo chochote kinachoashiria dharau kwa Mamlaka ya Spika.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilikutana rasmi kuanzia tarehe 7 Machi, 2016 hadi tarehe 12 Machi, 2016 na ilianza kushughulikia suala hilo.

Mheshimiwa Spika, wakati Kamati ilipokuwa ikiendelea na Kazi siku ya tarehe 10 Machi, 2016 uliielekeza Kamati kufanya uchunguzi kwa mashahidi wengine watatu ambao ni wafuatao;

Mhe.Zitto Zuberi Ruyagwa Kabwe,(Mb);

Mhe.John Heche,(Mb);na

Mhe.Halima J.Mdee, (Mb).

Aidha, katika maelekezo hayo, uliiagiza Kamati kufanya uchunguzi wa mwenendo mzima wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusiana na tukio la vurugu zilizotokea Bungeni tarehe 27 Januari, 2016.

Mheshimiwa Spika, mashahidi hao pia walipatiwa Hati za Wito zilizowataka kufika mbele ya Kamati na kutoa maelezo kuhusiana na tukio la vurugu zilizotokea siku ya tarehe 27 Januari, 2016.

CHIMBUKO LA SHAURI

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 27 Januari, 2016, katika Bunge la Kumi na Moja, Mkutano wa Pili, katika kikao cha asubuhi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Kanuni ya 49 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 alitoa kauli kuhusu Uamuzi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kusitisha kurusha matangazo ya moja kwa moja na badala yake alieleza kuwa vipindi hivyo vitaoneshwa katika kipindi Maalumu kinachoitwa “Leo Katika Bunge”.

Mheshimiwa Spika, baada ya Waziri wa Habari kutoa Kauli ya Serikali Bungeni, Mhe. Zitto Zuberi Ruyagwa Kabwe (Mb), alitoa hoja ya kuahirisha mjadala kupitia Kanuni ya 69 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016. Katika kujenga hoja yake Mheshimiwa Zitto (Mb) alimtaka Mwenyekiti kusitisha Mjadala wa kujadili hotuba ya Rais ya kulifungua Bunge ili kujadili kauli ya Mhe. Waziri kwa kuwa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya TBC ni

kuwazuia wananchi kufuatilia hoja za wabunge na kuwanyima wananchi haki ya kupata taarifa.


Mheshimiwa Spika, kufuatia hoja iliyowasilishwa na Mhe. Zitto Kabwe (Mb), Mhe. Andrew J. Chenge (Mb), Mwenyekiti alitoa mwongozo wake kuhusiana na hoja iliyotolewa ya kuahirisha Bunge kama ifuatavyo nanukuu:1

“Mwenyekiti: Waheshimiwa Wabunge, nimemsikiliza kwa makini Mheshimiwa Zitto Kabwe (Mb) kwa hoja yake ambayo msingi wake unaanzia Kanuni ya 49 ambayo inahusu kauli za Mawaziri. Kauli za Mawaziri kwa mujibu wa Kanuni hizi na kwa mujibu wa mazoea yetu hazijadiliwi Bungeni. (Makofi)

Hata hivyo, hilo halizuii Mbunge kuleta hoja substantive kupitia kwa Katibu kwa taratibu ambazo zimewekwa. Uamuzi wangu, kama Mheshimiwa Zitto Kabwe bado unaona umuhimu wa hoja hiyo kuendelezwa, nakushauri tu uzingatie hilo, ulete hoja hiyo kwa taratibu zilizopo. Kwa maana hiyo sasa, nachukua uamuzi kwamba kuahirisha mjadala ulio mbele yetu wa Hotuba ya Rais hautakuwa uendeshaji bora wa shughuli za Bunge.(Makofi)

Naagiza meza tuendelee. Mheshimiwa Bashungwa!”

Mwisho wa kunukuu.

1 Kumbukumbu Rasmi za Bunge za Tarehe 27 Januari, 2016 uk wa 70

Mheshimiwa Spika, Mhe. Andrew J. Chenge (MB.) alitoa Mwongozo kuwa, kwa kuzingatia misingi bora ya utaratibu wa uendeshaji wa Bunge, hakuona kama ingekuwa busara kuahirisha mjadala wa Hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kulifungua Bunge, badala yake alimshauri Mheshimiwa Zitto Kabwe (Mb) kufuata utaratibu mwingine wa kikanuni wa kuwasilisha hoja mahsusi kuhusu haki ya wananchi kupata habari za vikao vya Bunge kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Hivyo, Mwenyekiti aliamuru Bunge liendelee na shughuli kama zilivyopangwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya mwongozo huo baadhi ya Wabunge waliendelea kusimama na kuomba Mwongozo wa Mwenyekiti katika jambo ambalo lilikwisha amuliwa kutokana na hoja ya Mhe. Zitto kabwe (Mb). Wabunge hao waliendelea kuwasha vipaza sauti na kuzungumza bila utaratibu jambo lililopelekea Mwenyekiti kuahirisha kikao cha asubuhi ili kutoa nafasi kwa Kamati ya Uongozi kushauri namna ya kushughulikia suala husika.

Mheshimiwa Spika, mashauriano na Kamati ya Uongozi yalimwezesha Mwenyekiti kuwasilisha taarifa kwamba, Kamati ya Uongozi ilikubaliana na Mwongozo wa Mwenyekiti kwamba, kuahirisha kujadili Hotuba ya Rais haikuwa namna Bora ya Uendeshaji wa Shughuli za Bunge. Hata baada ya kutoa maelekezo hayo, bado baadhi ya wabunge waliendelea kusimama, kuomba mwongozo na kuongea bila kufuata taratibu za kikanuni. Jambo hili lilisababisha shughuli za Bunge zilizokuwa zimepangwa kwa siku hiyo kushindwa kuendelea kutokana na vurugu zilizokuwa zikiendelea.

Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti fujo hizo, Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia mamlaka yake chini ya Kanuni ya 74 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, aliwataja (Naming) baadhi ya Wabunge kuwa ndio walikuwa vinara wa kufanya vurugu na aliwataka watoke nje ya ukumbi wa Bunge. Wabunge waliotajwa ni Mhe. Godbless Lema, (Mb) Mhe. Tundu Lissu, (Mb) Mhe. Ester Bulaya (Mb) na Mhe. Pauline Gekul (Mb).

Mheshimiwa Spika, Hata baada ya kuwataka Wabunge hao watoke nje, walikaidi na vurugu ziliendelea hivyo, Mwenyekiti alilazimika kutumia Mamlaka yake chini ya Kanuni ya 76 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 kuahirisha kwa Muda Shughuli za Bunge kwa nia ya kudhibiti fujo. Aliamuru Mpambe wa Bunge (Sergeant-at armrs) kuwatoa ukumbini wabunge waliokuwa wametajwa.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na Wabunge waliotajwa kukaidi maelekezo ya Kiti, Mhe. Mwenyekiti aliagiza askari wengine wa Bunge kuingia ukumbini ili kudhibiti fujo zilizokuwa zikiendelea. Hata hivyo, baada ya kuona Kambi ya Upinzani ilikuwa inahusika katika kufanya fujo, Mwenyekiti aliamuru Wabunge wote wa upande wa Kambi ya Upinzani kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge.

UCHAMBUZI WA HOJA ZILIZOIBULIWA NA KAMATI KUHUSU FUJO/VURUGU ZILIZOTOKEA BUNGENI SIKU YA TAREHE 27 JANUARI, 2016

Mheshimiwa Spika, Katika Waraka wako ulioelekeza shauri hili kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ulirejea Fasili ya 4(1) (a) na (b) ya Nyongea ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016. Kwa urahisi wa rejea nanukuu Fasili ya Kanuni hiyo:

4 (1) Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itatekeleza majukumu yafatayo:-

Kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala yote ya Haki,Kinga na Madaraka ya Bunge yatakayopelekwa na Spika;

Kushughulikia mambo yanayohusu maadili ya Wabunge yatakayopelekwa na Spika.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Hati za Wito zilizotolewa kwa mashahidi kama ilivyoelezwa awali mashahidi wanne ambao ni Mhe. Godbless Lema (Mb), Mhe. Tundu Lissu (Mb), Mhe. Pauline Gekul (Mb), na Mhe. Ester Bulaya (Mb) walitakiwa kufika mbele ya Kamati siku ya tarehe 9 Machi, 2016 katika Ukumbi Na. 203 (Pius Msekwa) katika Ofisi Ndogo za Bunge Dar es salaam ili kujibu tuhuma zilizowakabili ambazo ni:-

Kusimama na kuomba mwongozo kuhusiana na jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi kinyume na Kanuni ya 72(1),na 68(10) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016;

Kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu kinyume na Kanuni ya 60(2) na (12) ya Kanuni za Bunge, Jambo ambalo lilileta fujo na kuvuruga shughuli za Bunge;

Kudharau mamlaka ya Spika kinyume na Kifungu cha 24 (c) (d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni ya 74(1) (a) na (b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Mheshimiwa Spika, kati ya mashahidi hao wanne, mashahidi watatu ambao ni Mhe. Lema (Mb), Mhe. Lissu (Mb) na Mhe. Pauline Gekul (Mb) waliitikia wito na walifika mbele ya Kamati siku ya Jumatano tarehe 9 Machi, 2016 kama walivyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, Mhe. Ester Bulaya (Mb) hakufika mbele ya Kamati na hapakuwa na sababu yoyote iliyofikishwa katika Kamati kuhusu kutofika kwake. Kwa Mujibu wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, Kamati ilimwandikia Spika kumjulisha kuhusu kutofika kwa Mhe. Ester Bulaya (Mb). Kwa kuwa ilithibitika kwamba Shahidi huyo alipokea hati ya Wito na kwamba hakufika Mbele ya Kamati bila kutoa sababu zozote. Baada ya Kamati kumwandikia Spika, Mhe. Spika aliridhika kuwa Shahidi amekaidi wito wa Kamati, hivyo alitoa Hati ya Kukamatwa kwake (Warant of Arrest). Hati hiyo ilikabidhiwa kwa IGP ambaye alimkamata Mhe. Esther Bulaya (Mb) katika Hotel ya Crest, Jijini Mwanza. Mh. Ester alifikishwa mbele ya Kamati Dar es salaam siku ya tarehe 11 Machi, 2016.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilipomhoji Mhe. Bulaya kwanini hakufika mbele ya Kamati alieleza kuwa alikuwa anaumwa na kwamba kwake yeye suala la afya yake lilikuwa muhimu zaidi kuliko kuhudhuria mbele ya Kamati. Kamati ilipomdadisi zaidi alieleza kuwa alikuwa Mwanza Kuhudhuria Mkutano wa Kamati Kuu ya Chadema kama mjumbe mwalikwa. Baada ya kupata maelezo hayo, Kamati ilisikitishwa na kitendo cha Mheshimiwa Bulaya kudharau wito wa Kamati.

Mheshimiwa Spika, Katika kutafakari jambo hili, Kamati iliainisha hoja za msingi ambazo zilihitaji kupata majibu ya Kamati ambazo ni:-

Iwapo ulikuwepo mwongozo wowote uliotolewa na Mwenyekiti wa Bunge baada ya Mhe. Zitto Kabwe kutoa Hoja ya kuomba kuahirishwa kwa Bunge kupitia Kanuni ya 69 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari, 2016? Jibu kama ni ndiyo je, Mashahidi waliofikishwa mbele ya Kamati walizingatia mwongozo huo?

Je, Mashahidi waliofikishwa mbele ya Kamati walisimama na kuzungumza bungeni bila kufuata utaratibu uliowekwa chini ya Kanuni ya 60(2) na (12)?

Je, Mashahidi waliofikishwa mbele ya Kamati walitamka maneno yoyote au kufanya vitendo vyovyote vya kudharau mamlaka ya Spika katika siku inayolalamikiwa?

Mheshimiwa Spika, katika kujibu hoja zilizoibuliwa na Kamati, Kamati imejielekeza kupata majibu ya hoja moja baada ya nyingine kama ifuatavyo:-

Iwapo ulikuwepo mwongozo wowote uliotolewa na Mwenyekiti wa Bunge baada ya Mhe. Zitto Kabwe kutoa Hoja ya kuomba kuahirishwa kwa Bunge kupitia Kanuni ya 69 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari, 2016? Jibu kama ni ndiyo je, Mashahidi waliofikishwa mbele ya Kamati walizingatia mwongozo huo?

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Kanuni ya 68(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Mwongozo wa Spika ni ufafanuzi ambao Kiti kinautoa kuhusu jambo linaloruhusiwa au kutoruhusiwa Bungeni na ambalo limetokea mapema bungeni.

Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 68(7) inaeleza, Nanukuu:

Hali kadhalika, Mbunge anaweza kusimama wakati wowote ambapo hakuna Mbunge Mwingine anayesema na kuomba “mwongozo wa Spika” kuhusu jambo ambalo limetokea Bungeni mapema, ili Spika atoe ufafanuzi kama jambo hilo linaruhusiwa au haliruhusiwi kwa mujibu wa Kanuni na taratibu za Bunge na majibu ya Spika yatatolewa papo hapo au baadaye kadri atakavyoona inafaa

Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 27 Januari, 2016 Mheshimiwa Zitto Kabwe alitoa hoja ya Kuahirisha kujadili Hotuba ya Rais ya Kulifungua Bunge na badala yake alitaka Bunge lijadili kauli ya Serikali iliyokuwa imetolewa na Mhe. Nape Mosses Nnauye (Mb), Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kusitisha Utangazaji wa moja kwa moja wa Matangazo ya Bunge uliokuwa ukifanywa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Mhe. Zitto alitoa hoja ifuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti2, kifungu cha (2) nakisoma kwa niaba yako, maana yake ulitakiwa ukisome wewe:” Kama Spika atakuwa na maoni kwamba kuwasilishwa kwa kwa hoja hiyo, ni kinyume cha uendeshaji bora wa shughuli za bunge, atakataa kuitoa ili iamuliwe. Vinginevyo papo hapo atawahoji wabunge juu ya hoja hiyo kadri atakavyoona inafaa

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitoe hoja yangu kwa nini naomba Bunge lako Tukufu, liahirishe mjadala wa Hotuba ya Rais mpaka hapo baadaye baada ya hoja ninayotoa. Muda mfupi uliopita, Waziri wa Habari ametoa kauli ya Serikali ambayo inawanyima haki wananchi ya kufuatilia shughuli za baraza lao la uwakilishi, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Televisheni ya Taifa (TBC) ni televisheni inayoendeshwa na fedha za Umma zinazopitishwa na Bunge. Walipakodi ndio wanaoendesha TBC. TBC si televisheni ya biashara, inafanya biashara kwa

2 Kumbukumbu Rasmi za Bunge za Tarehe 27 Januari, 2016 Uk wa 68 &69

sababu tu serikali imeshindwa kutoa mafungu yanayotosha ya kuendesha shughuli zake. TBC haiwezi kwa namna yoyote ile kuwanyima haki wananchi ya kufuatilia wawakilishi wao wanazungumza nini na wanafanya nini.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana kwa muda mrefu sasa kumekuwa na shughuli za Bunge zikioneshwa na Televisheni ya Taifa moja kwa moja. Kuendelea kujadili Hotuba ya Rais ambayo yeye wakati anahutubia ilioneshwa moja kwa moja. Kuwazuia Wananchi kufuatilia hoja za Wabunge kwa Hotuba ambayo Rais alipokuwa anahutubia ilikuwa moja kwa moja, ni kunyima haki za wananchi kupata taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Bunge lisitishe mjadala wa Hotuba ya Rais ambayo yeye alioneshwa moja kwa moja, lakini mhimili wa Bunge unapoijadili isioneshwe moja kwa moja, ili wabunge wajadili na watoe maazimio ambayo yatapelekea Serikali kuliachia Shirika la TBC lioneshe shughuli za Bunge moja kwa moja kwa mujibu inavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kutoa hoja.(Makofi)”

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 69(2)3 baada ya Hoja ya kusitisha mjadala, Spika au Mwenyekiti wa Bunge anayeongoza kikao kwa siku husika akiwa na maoni kwamba kuwasilishwa kwa hoja hiyo ni kinyume

3 Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016

cha uendeshaji bora wa shughuli za Bunge atakataa kuitoa hoja hiyo iamuliwe, vinginevyo, papo hapo atawahoji wabunge juu ya hoja hiyo kadri atakavyoona inafaa.

Mheshimiwa Spika, Mwenyekiti aliyekuwa anaongoza kikao siku ya tarehe 27 Januari, 2016 aliikataa hoja ya Mh. Zitto Kabwe na aliona kuwa, kuruhusu hoja yake ingekuwa ni kwenda kinyume cha uendeshaji bora wa shughuli za Bunge. Mwenyekiti alimshauri Mheshimiwa Zitto Kabwe kama bado alikuwa anaona hoja yake ilikuwa inafaa kujadiliwa na Bunge, awasilishe hoja yake kwa Katibu wa Bunge. Uamuzi wa Spika kuhusu Hoja ya Mheshimiwa Zitto Kabwe(Mb) ni ifuatayo:

Mwenyekiti4, Waheshimiwa Wabunge, nimemsikiliza kwa makini Mheshimiwa Zitto Kabwe kwa hoja yake ambayo msingi wake unaanzia kanuni ya 49 ambayo inahusu kauli za Mawaziri. Kauli za Mawaziri kwa mujibu wa Kanuni hizi na kwa mujibu wa mazoea yetu hazijadiliwi Bungeni. (Makofi)Hata hivyo, hilo halizuii Mbunge kuleta hoja substantive kupitia kwa Katibu kwa taratibu ambazo zimewekwa. Uamuzi wangu, kama Mheshimiwa Zitto Kabwe bado unaona umuhimu wa hoja hiyo kuendelezwa, nakushauri tu uzingatie hilo, ulete hoja hiyo kwa taratibu zilizopo. Kwa maana hiyo

4 Kumbukumbu Rasmi za Bunge za Tarehe 27 Januari, 2016 uk wa 70

sasa, nachukua uamuzi kwamba kuahirisha mjadala ulio mbele yetu wa Hotuba ya Rais hautakuwa uendeshaji bora wa shughuli za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 5 ya Kanuni za Kudumu za

Bunge5 inampa Mamlaka Spika ya kusimamia masuala yote yanayohusu utaratibu wa uendeshaji wa shughuli za Bunge na kwamba yeye ndiye mwenye mamlaka ya kutilia nguvu kanuni zote za Bunge. Kwa Mujibu wa Kanuni ya 68(10) na 72(1) ya Kanuni za Bunge6 uamuzi wa Spika kuhusu utaratibu wa uendeshaji wa shughuli za Bunge ni wa mwisho na haupaswi kuhojiwa isipokuwa kwa utaratibu uliowekwa kupitia Kanuni ya 5(4). Kanuni ya 68(10) na 72(1) zinaeleza ifuatavyo:

“Kanuni ya 68(10) Uamuzi wa Spika kuhusu suala lolote la utaratibu utakuwa ni wa mwisho.”

Kanuni ya 72(1) Spika atakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa, utaratibu bora unafuatwa bungeni, na uamuzi wa Spika kuhusu jambo lolote la utaratibu utakuwa ni wa mwisho”

Mheshimiwa Spika, Mwandishi maarufu wa masuala ya Bunge Eskine May7 anaeleza katika kitabu chake kuwa

5 Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 6 Toleo la Januari, 2016

7 Eskine May katika kitabu chake kiitwacho Parliamentary Practice, Toleo la 20

Maamuzi ya Maspika ni chanzo kimojawapo cha utaratibu unaopaswa kuzingatiwa katika uendeshaji wa Bunge. Maamuzi ya Spika ndani ya Bunge au Mwenyekiti wakati wa Kamati ya Bunge zima huwa na nguvu ya kisheria na hadhi sawa na maamuzi ya kimahakama na hupasa kuzingatia mifumo ya ulinganishi wa maamuzi yaliyopata kutolewa siku za awali. Utaratibu huu hupasa kwenda sambamba uzingatiaji wa Sheria na Kanuni za Bunge.

3.15 Mwandishi Eskine anaeleza ifuatavyo:

The third source of procedure in the House is to be found in the rulings from the chair. Recuring to the previously mentioned analogy with the general law, if ancient usage correspondes to the Common Law and Standing Orders to the Statute Law,the rulings of the Speaker in the House, and of the Chairman in the Committee of the Whole House, afford an obvious parallel to the decisions of Judges in the Courts.

Mheshimiwa Spika, Katika utaratibu wa uendeshaji wa vikao vya Bunge katika mabunge yote Duniani, Uamuzi wa Spika au Mwenyekiti kuhusu masuala yote ya utaratibu huwa ni wa mwisho. Ifuatayo ni Mifano michache ya Kanuni za baadhi ya Mabunge:

3.17 Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Ghana Kanuni ya 988 inatambua kwamba Spika ndiye anawajibika katika kusimamia masuala ya utaratibu na majadiliano Bungeni na uamuzi wa Spika unakuwa ni wa mwisho na kwamba hautakiwi kupingwa mahakamani au bungeni isipokuwa pale ambapo itatolewa hoja mahsusi baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya kusudio la kufanya hivyo. Kanuni hiyo inaeleza ifuatavyo:

Mr. Speaker shall be responsible for the observance of order in the House and of the rule of debate, and his decision upon any point of order shall not be open to appeal and shall not be reviewed by the House, except upon a substantive motion made after notice

3.18 Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Lok Sabha, India Kanuni ya 3789 inaeleza kuwa Spika wa Bunge ndiye mwenye mamlaka ya kusimamia masuala yote ya utaratibu Bungeni. Kanuni hiyo inaeleza ifuatavyo;

The Speaker shall preserve order and shall have all powers necessary for purpose of enforcing his decisions

3.19 Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, Mheshimiwa Mwenyekiti alikuwa ametoa mwongozo wake kuhusiana na Hoja iliyokuwa imetolewa na Mhe.

8 Kanuni za Kudumu za Bunge la Ghana, Toleo la Tarehe 1 Novemba, 2000

9 Kanuni za utaratibu na uendeshaji wa Shughuli za Bunge la Lok Sabha, Toleo la Tisa

Zitto Kabwe. Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na kwa kuzingatia kuwa Spika ndiye mwenye mamlaka ya mwisho kuhusu utaratibu Wabunge wote walipaswa kuzingatia Mwongozo huo uliotolewa na Spika.

Mheshimiwa Spika, Kati ya Mashahidi saba waliopewa hati za Wito kuhusiana na jambo hili ni mashahidi watano ndio waliohojiwa na Kamati ambao ni: Mhe. Ester Bulaya (Mb), Mhe, Halima Mdee (Mb), Mhe. Zitto Kabwe (Mb) na Mhe. John Heche (Mb). Mhe. John Heche alifika mbele ya Kamati na Wakili wake Mhe. James Ole Milya (Mb). Hata Hivyo, Kwa mujibu wa taratibu za kibunge, Mhe. James Ole Milya (Mb) hakuruhusiwa kuongea na Kamati bali alishauriana na mteja wake kabla na wakati wa mahojiano na Kamati.

Mheshimiwa Spika, mashahidi watatu hawakuhojiwa. Mashahidi ambao hawakuhojiwa na Kamati ni watatu ambao ni Mhe. Tundu Lissu (Mb), Mhe. Godbless Lema na Mhe Pauline Gekul (Mb). Mashahidi hawa walifika mbele ya Kamati siku ya tarehe 9 Machi, 2016 Dar es Salaam kama walivyotakiwa Hata hivyo, hawakuhojiwa kwa kuwa waliomba muda zaidi wa kushauriana na Mawakili. Kamati ilijadili maombi yao, iikaridhia na kuwataka kufika mbele ya Kamati siku ya tarehe 11 Machi, 2016.Hata hivyo,

Mashahidi hawa hawakufika mbele ya Kamati na hawakutoa taarifa yoyote hadi Kamati inakamilisha kazi yake.

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 13(6) ya Katiba10 inatoa wajibu kwa mamlaka zote zinazohusiana na utoaji haki kuzingatia misingi muhimu iliyowekwa na Katiba wakati wa kutekeleza wajibu wa kutoa haki. Ibara hiyo inasomeka kama ifuatavyo; nanukuu

Kwa madhumuni ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria, mamlaka ya nchi itaweka taratibu zinazofaa au zinazozingatia misingi kwamba-

wakati wa haki na wajibu kwa mtu yoyote inapohitajika kufanyiwa uamuzi na mahakama au chombo kingine chochote kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kikamilifu, na pia haki ya kukata rufani au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo hicho kinginecho kinachohusika.”

Mheshimiwa Spika, kutokana na masharti ya Ibara hiyo, haki ya mtu kusikilizwa kikamilifu ni pamoja na kupata fursa ya kuwa na Wakili wakati wa kujitetea. Kwa mujibu wa Kifungu cha 26 cha Sheria inayozungumzia Kinga Haki na

Madaraka ya Bunge11 mwenendo wa mashauri katika Bunge au Kamati ya Bunge humtaka mtu anayetoa ushahidi au kuwasilisha nyaraka kwa kufuata utaratibu sawa na unaotumika katika Mahakama.

Mheshimiwa Spika, Mwandishi Eskine May12 anaeleaza katika kitabu chake kuwa, wanaotuhumiwa kwa uvunjaji wa haki na kinga za Bunge kwa ujumla hawaruhusiwi kuwakilishwa na wakili, hata hivyo, wanaweza kuwakilishwa na Mawakili wao katika mazingira fulani fulani.

nukuu:

Persons accussed of breaches of privileges or other contempts of either house are not, as a rule, allowed to be defended by a counsel but in a few cases incriminated persons are allowed to be heard by a counsel, the hearing sometimes limited to such points as do not controvert the privileges of the House

Mheshimiwa Spika, ni kwa kuzingatia misingi ya Katiba na Sheria pamoja na uzoefu wa mabunge mengine duniani, Kamati iliamua kutoa fursa kwa mashahidi walioomba kupewa fursa ya kupata mawakili. Mashahidi hao ni Mhe. Tundu Lissu (Mb), Mhe.Godbless Lema (Mb) na Mhe. Pauline Gekul (Mb). Kamati iliwapa muda wa Siku mbili toka tarehe 9 machi hadi tarehe 11 Machi, 2016 ili kuwawezesha kupata mawakili kama ilivyoombwa.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 226 (1) cha Sheria ya

Mwenendo wa Makosa ya jinai13 kinaeleza kuwa, endapo mtuhumiwa atakuwa amepewa taarifa ya mahali, siku na muda wa shauri kuendelea kusikilizwa na ataamua kutofika mahakamani, mahakama inaweza kuendelea bila ya yeye kuwepo.

Mheshimiwa Spika, mashahidi hao watatu hawakufika siku iliyopangwa na pia hawakuwahi kuwasilisha maelezo yoyote mbele ya Kamati kuhusu sababu za kushindwa kufika mbele ya Kamati kutokana na sababu hiyo, na kwa kuzingatia kuwa mashahidi wote walipewa fursa ya kutosha ya kusikilizwa, na walifahamishwa kwamba wakishindwa kufika siku iliyopangwa Kamati itaendelea na kazi yake. Kamati iliamua kuendelea kujadili suala lililowakabili Mashahidi hao hata bila ya wao kuwepo. Vikao vya Kamati kujadili suala hili viliendelea tena Dodoma kuanzia tarehe 16 Mei, 2016 hadi kukamilika kwake. Hicho ni kipindi cha miezi miwili na siku mbili tangu vikao hivyo kuahirishwa.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kujikita katika kosa la kwanza ambalo mashahidi walishitakiwa nalo. Kosa hilo linasomeka kama ifuatavyo,

Kusimama na kuomba mwongozo kuhusiana na jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi kinyume na Kanuni ya 72(1), na 68 (10) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo na ufafanuzi uliotolewa hapo juu na kwa kuzingatia mamlaka ya kikanuni aliyonayo Spika, mara baada ya Mwenyekiti kutoa mwongozo na kuagiza shughuli iliyokuwa mezani kwa siku hiyo iendelee, wabunge wote walipaswa kuheshimu Kiti na kuendelea na shughuli iliyokuwa mezani. Katika Ukurasa wa 70 wa Kumbukumbu Rasmi za Bunge za siku hiyo (Hansard) Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kikao cha siku husika alisikika akisema yafuatayo;

Nimeagza meza tuendelee14. Mheshimiwa Bashungwa!

Mheshimiwa Spika, Kutokana na Mheshimiwa Mwenyekiti kumruhusu Mhe. Bashungwa atoe mchango wake, Wabunge wote walipaswa kutii, kutulia na kumuacha achangie. Suala hilo halikutekelezwa kwani mahahidi waliendelea kufanya vurugu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Halima James Mdee (Mb) alipofika mbele ya Kamati alikana kuhusika na kosa la kwanza la kusimama na kuomba mwongozo kwa Jambo ambalo lilikwishatolewa uamuzi kinyume na Kanuni ya 72(1) na 68(10). Aidha, Mhe. Halima Mdee (Mb) aliieleza Kamati kwamba alisimama kuomba mwongozo na Mhe. Mwenyekiti alimruhusu baada ya kuona hoja yake ni ya msingi na baada ya hapo Mwenyekiti aliahirisha Bunge. Alieleza pia kuwa, yeye pamoja na Mhe. Zitto Kabwe (Mb) walifika mbele ya Kamati ya Uongozi na wakaeleza hoja zao. Baada ya hapo alisema kuwa hakuomba mwongozo wowote na kwamba, katika kikao cha jioni hakuingia ukumbini isipokuwa aliingia mwishoni kabisa wakati vurugu zilikwisha anza na wala hahusiki na vurugu hizo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Mhe. Halima Mdee (Mb) aliieleza Kamati kwamba anachojua ni kwamba, suala lake lilikwisha mara baada ya Kamati ya Uongozi kukaa na kutoa ufafanuzi kuhusu hoja yake hivyo alieleza kuwa kuitwa tena katika Kamati ni kufufua jambo ambalo lilikuwa limekwisha. Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya uchambuzi wa utetetezi wa Mheshimiwa Halima James Mdee(Mb) Kama ifuatavyo;

Ilidhihirika kuwa, katika Ukurasa wa 70 wa Hansard, Mhe. Mwenyekiti alikuwa ameshatoa uamuzi kuhusu hoja iliyokuwa imetolewa na Mhe. Zitto (Mb) kwa kueleza kuwa kusitisha kujadili Hotuba ya Rais ya Kulifungua Bunge haikuwa utaratibu bora wa uendeshaji bora wa Shughuli za Bunge na kwamba tayari alikuwa amemwita Mhe. Bashungwa (Mb) kuendelea kuchangia. Kitendo cha Mhe.Halima Mdee (Mb) kuendelea kutaka kutoa hoja ya Haki za Bunge ilikuwa ni kuzungumzia jambo ambalo limekwisha amuliwa.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mahojiano yanayopatikana katika ukurasa wa 70 mpaka 71 wa Kumbukumbu Rasmi za Bunge, Mhe. Halima Mdee (Mb) alikuwa anabishana na Kiti jambo ambalo ni uvunjifu wa kanuni. Kitendo hicho kiliendelea hata baada ya Mwenyekiti kumsihi mara kwa mara jambo ambalo hakulitekeleza.

Mheshimiwa Spika, aidha, Mheshimiwa Mwenyekiti alikuwa amekwisha muita mchangiaji mwingine aliyekuwa amepangwa kuchangia kwa siku hiyo ili shughuli za Bunge

za siku hiyo ziendelee. Mchangiaji huyo alishindwa kuendelea kutokana na Mhe. Halima Mdee (Mb) kuendelea kushinikiza madai yake.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba Mh. Mdee alisimama kwa kutumia Kanuni ya 55(2) inayohusu Haki za Bunge, lakini msingi wa hoja yake ulikuwa ni kulitaka Bunge kuacha kujadili hoja ya Hotuba ya Rais ya Kulifungua Bunge jambo ambao lilikuwa ni kuombea mwongozo katika jambo ambalo lilikwishatolewa uamuzi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Halima Mdee (Mb) amenukuliwa akisema ifuatavyo katika ukurasa wa 73 wa

Hansard; nukuu:

MHE: HALIMA J. MDEE:

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna shughuli muhimu zaidi ya wananchi kusikiliza tunazungumza nini.”

Kauli hii ya Mhe. Mdee inadhihirisha ukweli kuwa alikuwa anaendelea kupingana na umamuzi wa kiti na kwamba alikuwa anamshinikiza Mhe. Mwenyekiti. Aidha, Mhe. Halima Mdee amenukuliwa akitamka maneno; ”Ni hivi, usitutishe”, usituburuze bwana!”. Kauli na maneno haya ni ukiukaji wa Kanuni na yalitumika ili kutumia nguvu kutaka kulazimisha utaratibu wa kuendesha Bunge badala yakuzingatia kanuni. Isitoshe, lugha hiyo aliyotumia Mhe. Halima Mdee siyo lugha ya kibunge ukizingatia kuwa yeye ni Mbunge mzoefu anayejua fika Kanuni na matumizi yake.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo, Kamati imemkuta na hatia Mhe. Halima James Mdee (Mb) kwa kosa la kusimama na kuomba mwongozo katika jambo ambalo lilikuwa limeombewa na kutolewa mwongozo.

Mheshimiwa Spika, Shahidi mwingine aliyehojiwa ni Mhe. John Heche (Mb). Alipoulizwa kuhusu kutenda kosa kwa kuomba mwongozo katika jambo ambalo lilikuwa limekwishatolewa uamuzi, aliieleza Kamati kwamba sio kweli kwasababu Mhe. Zitto Kabwe alikuwa ameomba mwongozo unaohusu Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) kutorusha matangazo ya shughuli za Bunge moja kwa moja wakati yeye aliomba mwongozo uliohusu uvunjwaji wa Katiba ya Nchi.

Mheshimiwa Spika, Katika maelezo yake alisema, ibara ya 18 ya Katiba inayotoa fursa ya wananchi kupata habari ilikuwa imevunjwa kwa kitendo cha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoa taarifa ya TBC kusitisha matangazo ya moja kwa moja. Aidha, alieleza kuwa mara baada ya kuruhusiwa kuomba mwongozo aliketi chini na hakuomba tena mwongozo wowote.

Mheshimiwa Spika, kama ilivyofafanuliwa hapo juu, Uamuzi wa Spika kuhusiana na suala la hoja ya Mhe. Zitto Kabwe (Mb) ya kulitaka Bunge kusitisha kujadili Hotuba ya Rais ulikuwa umekwishatolewa hata hivyo, Mh. Heche (Mb) alisimama na kuomba mwongozo kama ifuatavyo;

nanukuu:

MHE. JOHN W. HECHE:

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru,

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba yetu ibara ya 18, ukisoma kifungu (b) ya Katiba yetu inasema:

Kila mtu kwa maana ya kila mwananchi, anayo haki ya kupewa taarifa, wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri, tuko hapa kujadili masuala muhimu yanayohusu maisha ya wananchi wetu na tuko hapa kujadili masuala yanayohusu maisha ya wananchi wetu. Sasa hii ni Katiba, sisi tutakuwa watu wa ajabu kukubali kukaa humu ndani kuvunja Katiba, kuzuia wananchi kupata taarifa inatohusu Bunge lao na inayohusu maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba mwongozo wako, kama ni sahihi kukaa humu kujadili mambo

yanayovunja katiba, kwa sababu hapa sisi kwenda live kwa televisheni ya Taifa, ambayo inalipiwa kodi zetu na hakuna kitu chochote kinachoongezeka, watumishi wanalipwa na mshahara wa Serikali sasa, hatujui hizo gharama anazozisema Mheshimiwa Nape, zinatoka wapi? Naomba mwongozo wako.”

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Mheshimiwa Heche (Mb) alitumia Ibara ya 18 ya Katiba kujenga hoja yake lakini mantiki na msingi wa hoja yake ulikuwa bado ni kujadili suala ambalo kiti kilikwisha kutoa uamuzi. Kimsingi, Mheshimiwa Heche alikuwa anataka Mhe. Mwenyekiti atoe uamuzi wa kuahirisha kujadili Hotuba ya Rais ya kulifungua Bunge suala lililokuwa mezani kwa wakati huo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo hayo yanayothibitisha kwamba Mh. John Heche amekiuka Kanuni, Kamati inamtia hatiani Mhe. John Heche kwa kosa la kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo lilikwishaamuliwa na Mwenyekiti.

Mheshimiwa Spika, Shahidi mwingine aliyehojiwa na Kamati alikuwa Mhe. Zitto Ruyagwa Zuberi Kabwe (Mb). Katika maelezo yake, kuhusu kosa la kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo lilikuwa limekwishatolewa uamuzi, alikana kuhusika na kutenda

kosa hilo. Mhe. Zitto aliieleza Kamati kuwa yeye hakuomba mwongozo kama hati ya Wito ilivyoeleza bali alitoa hoja ya kuahirisha mjadala kwa mujibu wa Kanuni ya 69 ya Kanuni za Kudumu za Bunge. Aidha, Mheshimiwa Zitto alileza kuwa baada ya kuruhusiwa kutoa hoja hiyo na baada ya Mwenyekiti wa Bunge kutoa mwongozo wake, alitii na hakuendelea tena kusimama au kuomba mwongozo wowote.

Mheshimiwa Spika, Baada ya Kamati kufanya uchambuzi wa Hansard ilibaini kuwa Mhe. Zitto hakuomba tena mwongozo au kutoa hoja nyingine yoyote mara baada ya Mwenyekiti kumshauri kuwa endapo aliona hoja yake ni Muhimu angeweza kuwasilisha hoja hiyo kupitia utaratibu mwingine.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uchambuzi wa Kamati, Mhe. Zitto Kabwe (Mb) alionekana kutotenda kosa la kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo lilikuwa limekwishatolewa uamuzi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo hayo, Kamati inamuona Mh. Zitto hakutenda kosa hilo.

Mheshimiwa Spika, Shahidi mwingine alikuwa Mhe. Ester Bulaya (Mb), ambaye baada ya kuulizwa na Kamati kuhusu kitendo chake cha kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo lililokwisha kutolewa uamuzi na Mwenyekiti, aliieleza Kamati kuwa ni kweli yeye alisimama kutaka kuomba mwongozo na kwamba Kanuni zinaruhusu mbunge yeyote kusimama mahali pake na kuomba mwongozo. Mhe. Ester Bulaya aliendelea kusema kuwa yeye alikuwa anataka kuomba mwongozo katika jambo lingine na sio lililokuwa limetolewa uamuzi. Aidha, Mhe. Ester Bulaya (Mb) alisema kuwa pamoja na yeye kusimama ili apate fursa ya kuomba mwongozo lakini hakupewa fursa hiyo.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya rejea ya Hansard kuona Kama Mhe. Ester Bulaya (Mb) aliomba mwongozo. Ilibainika kuwa hakuna sehemu yoyote katika Hansard inayoonesha kuwa alisimama na kuomba mwongozo hivyo, Kamati haikumuona na kosa hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mhe. Godbless Lema (Mb) Kamati ilifanya uchambuzi kuhusu kusimama kwake na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo tayari limekwisha amuliwa kinyume na Kanuni ya 72(1) na 68(10) ya Kanuni. Kamati ilibaini kuwa hakuna sehemu yoyote katika Hansard inayoonesha kuwa Mhe. Lema alisimama na kuomba mwongozo. Kutokana na ushahidi huo, Kamati haikumuona Mhe. Godbeless Lema kuwa na hatia katika kosa la kwanza lililoainishwa katika hati ya wito.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mhe Pauline Gekul (Mb) Kamati ilifanya rejea katika ukurasa wa 83 wa Hansard na kubaini kuwa aliendelea kusimama na kuomba mwongozo katika jambo ambalo lilikwishakutolewa uamuzi. Kumbukumbu

hizo zinasomeka kama ifuatavyo, nanukuu:

MHE. PAULINE P. GEKUL15: Mwongozo wa Mwenyekiti.

WABUNGE FULANI: Aaaa!

MWENYEKITI: “INNOCENT BASHUNGWA!”

PAULINE GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo wako kuhusu utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti Naomba Mwongozo wako kuhusu utaratibu kwa Kanuni ya arobaini…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gekul, nawasihi sana Waheshimiwa Wabunge, nimefafanua uamuzi wa Kamati ya Uongozi, nimeusoma kama ulivyo, nimefafanua baada ya ombi la mwongozo wa Mhe. Tundu Lissu(Mb)

Waheshimiwa Wabunge, Hatua inayofuata sasa ni kwenda mbele, mjadala huu uendelee na kama yapo makandokando ambayo yamejificha kupitia uamuzi (Makofi)…….

MHE: PAULINE GEKUL: “, Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nahitaji mwongozo wako kupitia utaratibu wa Kanuni ya 49 ambao ni wa Kauli za Mawaziri. Naomba

tu nisome(42(2) inasema hivi” kauli za aina hiyo zinaweza kutolewa kwa idhini ya Spika, katika wakati unaofaa, kufuatana na mpangilio wa shughuli za Bunge na zitahusu jambo mahsusi, halisi na zisizozua mjadala na muda wa kusema utakuwa ni dakika zisizozidi thelathini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kauli ya Waziri aliyoitoa asubuhi imezua mjadala, Kanuni yetu inasema kwamba hizo kauli zao zisizue mjadala, ni kwanini unakataa shughuli za Bunge zisiahirishwe, tujadili kauli hiyo ambayo imezua mjadala? Wakati Kanuni ime-restrict kwamba issue isizue mjadala? Naomba mwongozo wako. (Makofi)”

Mheshimiwa Spika, kama inavyojidhihirisha, Kamati inaridhika kuwa, Maelezo ya Mwongozo wa Mhe. Gekul (Mb) yalikuwa ya kuvuruga shughuli za Bunge kwa kuwa, tayari uamuzi wa jambo alilokuwa analiombea Mwongozo ulikuwa umetolewa.

Mheshimiwa Spika, Kamati inamtia Hatiani Mhe. Gekul (Mb) kwa kosa na kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo lilikuwa limekwishakutolewa uamuzi.

Mheshimiwa Spika, Mhe. Tundu Lissu (Mb) katika hati yake ya mashtaka , kosa la kwanza lilikuwa kuendelea kusimama na kuomba mwongozo katika jambo ambalolilikwisha kutolewa uamuzi kinyume na Kanuni ya 72(1) na Kanuni ya 68(10).

Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya uchambuzi wa kumbukumbu rasmi za Bunge na kubaini kuwa Mh. TunduLissu alijihusisha na uvunjwaji huo wa Kanuni. Katika kutafakari, Kamati ilifanya rejea katika Uk wa 84. Mhe Lissu anasema:

nukuu:

MHE. TUNDU A.M.LISSU: Mwongozo wa Mwenyekiti16….

Aidha katika ukurasa wa 8517 mahojiano yanasomeka kama ifuatavyo;

MHE: TUNDU A. LISSU: Simameni basi.

MWENYEKITI: Ni mwongozo tu, wote mnataka mwongozo?

WABUNGE FULANI : Ndiyo.

MWENYEKITI: Unafanana na hili alilolisema Mheshimiwa Heche?

MHE: TUNDU A. M. LISSU: Si mnataka mwongozo, simameni muombe mwongozo.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naona sasa tunataka kutumia utaratibu wa kuchelewesha shughuli za Bunge.

MHE. TUNDU A.M. LISSU: Mwongozo, mwongozo, tunataka mwongozo

MWENYEKITI: Nimesimama.

TUNDU A.M. LISSU: Mwongozo

MWENYEKITI: Nimesimama

MBUNGE FULANI: Hatuwezi kukubali Katiba inavunjwa

MWENYEKITI: Nimesimama nawasihi mketi.”

Mheshimiwa Spika, mtiririko wa mahojiano hayo kati ya Mhe. Lissu na Mwenyekiti unaonesha kuwa Mhe. Lissu aliendelea kusimama na kuomba mwongozo hata baada ya umauzi wa jambo alilokuwa analiombea Mwongozo kutolewa. Aidha, Mhe. Lissu ambaye ni mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alihamasisha wabunge wengine kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo siyo tu ni kinyume cha Kanuni, bali pia lilihamasisha vurugu Bungeni.

Mheshimiwa Spika, Kutokana ushahidi uliowasolishwa kuwa mbele ya Kamati na kwa ufafanuzi wa uvunjifu huo wa Kanuni, Kamati inamtia hatiani Mhe. Tundu Lissu kwa kosa la kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishaombewa Mwongozo na kuamuliwa.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kujielekeza katika suala la pili ambalo ni:

Iwapo mashahidi waliofikishwa mbele ya Kamati walisimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu kinyume cha Kanuni ya 60(2) na (12).

Kwa mujibu wa Kanuni ya 60(2) ya Kanuni za Bunge18 Mbunge hapaswi kuanza kuzungumza kabla ya

kuruhusiwa na Spika. Kanuni hiyo inaeleza: nukuu:

“60(1) Mbunge akitaka kusema anaweza:-

Kumpelekea Spika ombi la Maandishi;

Kusimama kimya mahali pake;au

Kutumbukiza kadi ya kielektroniki.

Isipokuwa kwamba, Mbunge yeyote hataanza kuzungumza hadi aitwe na Spika ama kwa jina au wadhifa wake na kumruhusu kusema na wakati wa kusema ataelekeza maneno yake kwa Spika”.

Mheshimiwa Spika, Kanuni hiyo inaweka utaratibu wa Mbunge kupata nafasi ya kuzungumza. Katika utaratibu huo Mbunge anaweza kumwandikia Spika akiomba fursa ya kuzungumza kusimama kimya mahali pake au kutumbukiza kadi ya kielektroniki. Mara nyingi njia zinazotumika ni kumpelekea Spika Ombi la Maandishi au kusimama kimya mahali pake ili Spika amuone na kumruhusu kuzungumza.

Mheshmiwa Spika, aidha, Kanuni ya 60(12) inaelekeza kuwa Spika anaposimama Waziri au Mbunge yeyote atakayekuwa anazungumza au aliyekuwa anasubiri kuanza kuzungumza anapaswa kuketi na kukaa kimya ili Spika aweze kutoa maelekezo au taarifa yake.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilimhoji Mhe. Halima Mdee (Mb) kuhusu kosa la kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu na alikana kutenda kosa hilo. Mhe. Halima Mdee aliieleza Kamati kuwa alichokifanya ni kuomba mwongozo na baada ya kuruhusiwa kuwasilisha hoja yake alikaa na hakufanya jambo lolote kinyume cha taratibu. Aidha Mhe. Halima Mdee aliieleza Kamati kuwa baada ya Bunge kuahirishwa alienda kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi pamoja na Mhe. Zitto Kabwe kuwasilisha hoja zao

ambazo Mwenyekiti aliziona kuwa zilikuwa za msingi na kwamba baada ya hapo hakurudi ukumbini katika kikao cha jioni.

Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoeleza hapo awali, Kanuni ya 60 inafafanua utaratibu wa kupata nafasi ya kuzungumza. Katika Kumbukumbu rasmi za Bunge majadiliano yalikuwa hivi:


“MWENYEKITI: Tunaendelea19

MHE:HALIMA J.MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hoja kuhusu Haki za Bunge.

MWENYEKITI: Bashungwa, Mheshimiwa Bashungwa

MHE. INNOCENT BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti…..

MHE: HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti Hoja kuhusu Haki za Bunge!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima, nakusihi keti, keti”.

Mheshimiwa Spika, Kumbukumbu hizi zinathibitisha kuwa Mheshimiwa Halima Mdee alikuwa anazungumza pasipo kuruhusiwa na Kiti na alifanya hivyo wakati aliyekuwa ameruhusiwa ni Mhe. Innocent Bashungwa. Aidha Mhe. Mwenyekiti alimsihi Mhe. Halima na wabunge wengine kuketi yapata mara kumi ili Mhe. Bashungwa aendelee kuchangia. Ushahidi unaonesha kuwa Mhe. Mdee alikaidi maelekezo hayo na aliendelea kuzungumza.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mhe. Halima Mdee alikiuka Masharti ya Kanuni za Bunge. Mh. Mdee alikaidi wito wa Mwenyekiti wa kumtaka aketi na pia kwa kutamka

maneno msitutishe, msituburuze20 ambayo si maneno yanayokubalika katika lugha ya kibunge. Ushahidi wa lugha hiyo isiyokubalika upo katika ukurasa wa 72 na 73 wa Hansard. Kutokana na ushahidi huo, Kamati imenamtia

hatiani Mhe. Halima Mdee kwa kosa na kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu, Kamati ilimhoji Mhe. Zitto Kabwe kwa kutokana na vitendo vyake katika siku hiyo. Mhe. Zitto Kabwe aliieleza Kamati kuwa yeye alifuata utaratibu na hana kosa lolote hivyo, hana kosa la kujibu mbele ya Kamati. Mhe. Zitto Kabwe alieleza kuwa Kamati ilikuwa inampotezea muda wake kwa kumuita na kumhoji katika jambo ambalo hahusiki nalo.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya uchambuzi wa ushahidi uliotolewa na Mh. Zitto Kabwe na kulinganisha na Hansard ili kujiridhisha kama alitenda au hakutenda vitendo vinavyolalamikiwa vya kuzungumza bila kufuata utaratibu wa kikanuni. Katika uchambuzi huo, Kamati ilifanya rejea katika ukurasa wa 63, 64, 65 na 66 wa Hansard. Katika kurasa hizo mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo: nukuu:

MHE. KABWE Z.R ZITTO: hoja ya hadhi ya Bunge, Mheshimiwa Spika.

SPIKA: Naomba waheshimiwa Make

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, Hoja ya Hadhi ya Bunge

SPIKA: Naomba sana mkae, naomba nichukue nafasi hii kumkaribisha mwenyekiti, Mheshimiwa Andrew Chenge ili aendelee na ratiba iliyoko mezani. Mheshimiwa Chenge! (Makofi)

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kuahirisha mjadala.………

MHE. KABWE Z.R. ZITTO: Hoja ya kuahirisha mjadala, kanuni ya 69.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Innocent Bashungwa

MHE. INOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya….

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Kanuni ya 69, Mheshimiwa Mwenyekiti.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Zitto Nakusihi sana, hiyo Kanuni ya haki za Bunge hailazimishi kiti kikubali kama ilivyo, nakusihi isome vizuri (Makofi)

MHE: KABWE Z. R. ZITTO: Kanuni ya 69 hoja ya kuahirisha mjadala Mheshimiwa Mwenyekiti.”

Mheshimiwa Spika, mahojiano hayo yanadhihirisha ni kwa kiasi gani Mhe. Zitto alivyokaidi maelekezo ya kiti. Mwenyekiti alimsihi mara kadhaa kwamba aketi lakini hakutaka kutii. Ijapokuwa Mhe. Mwenyekiti alikuwa amemruhusu Mhe. Bashungwa kuchangia hakuweza kufanya hivyo kutokana na ukaidi uliofanywa na mheshimiwa Zitto Kabwe wa kuzungumza kinyume cha Kanuni.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ushahidi na maelezo hayo, Kamati inamtia hatiani Mhe. Zitto Kabwe kwa kosa la kuendelea kusimama baada ya kutakiwa na Kiti kuketi na kwa kuzungumza

bila kufuata utaratibu kinyume na kanuni ya 60(2) na (12) ya Kanuni za Bunge.

Mheshimiwa Spika, Katika uchambuzi wake Kamati ilipima ushahidi kuhusiana na ushiriki wa Mhe. Heche (Mb) na Mhe. Lema (Mb) katika suala hili na kubaini kuwa, ushahidi uliopo hauthibitishi kuhusika kwa wabunge hawa kuzungumza bila utaratibu kwa mujibu wa Kanuni ya 60. Kutokana na sababu hiyo, Kamati haikuwaona na kosa.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilijiridhisha na kujithibitishia kuwa, Mhe. Lissu (Mb) na Mhe Gekul (Mb) walikuwa wanazungumza bila ya kupewa ruhusa na Mhe. Mwenyekiti kinyume na Kanuni za Bunge. Mhe. Gekul kwa mujibu wa Hansard katika ukurasa wa 82 na 83 alizungumza wakati Mwenyekiti ameshamruhusu Mhe. Bashungwa kuzungumza jambo ambalo lilikuwa ni kuleta vurugu bungeni.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika ukurasa wa 83 wa Hansard Mhe. Lissu amethibitika kuwa alizungumza bila kufuata utaratibu. Ushahidi huo upo pia katika ukurasa wa 86 wa Hansard.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ushahidi na maelezo hayo, Kamati imewatia hatiani Mhe. Gekul (Mb) na Mhe. Lissu(Mb)kwa kosa la kusimama na kuzungumza kinyume na Kanuni za Bunge.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba tujielekeze katika kufanya uchambuzi wa suala kosa la tatu ambalo lilihusu:

Kudharau mamlaka ya Spika kinyume na Kifungu cha 24

(d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni ya 74(1) (a) na (b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 24(c), (d)

na (e) cha Sheria ya Haki na Kinga za Bunge21 ni kosa kwa mtu yeyote kuzuia au kuleta usumbufu katika maeneo ya Bunge wakati vikao vya Bunge au Kamati vinapokuwa vinaendelea, au kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu kwa Spika au kufanya kitendo chochote kwa makusudi, kudharau shughuli za Bunge au mtu anayeendesha shughuli hizo.

4.19 Mheshimiwa Spika, kwa urahisi wa rejea naomba kunukuu kifungu hicho;

“24. Any person shall be guilty of an offence who-(a) N/A

N/A

Causes an obstruction or disturbance within the precincts of the Assembly Chamber during a sitting of the Assembly or of the Committee thereof; or Shows disrespect in speech or manner towards the Speaker; or Commit any other act of intentional disrespect to or with reference to the proceedings of the Assembly or to any person presiding at such proceedings.

Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 74(1) nayo inakataza wabunge kufanya vitendo vyovyote ambavyo ni vya utovu wa nidhamu kwa Spika au Mtu yeyote anayeongoza kikao. kanuni hiyo inaeleza: nukuu:

“Spika anaweza kutaja jina la Mbunge kwamba amedharau mamlaka ya Spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ikiwa:-

Kwa maneno au kwa vitendo, mbunge huyo anaonesha dharau kwa mamlaka ya Spika;au

Mbunge huyo atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au mbunge yoyote anayeongoza shughuli hiyo”.

Meshimiwa Spika, Utaratibu ndani ya Bunge upo kwenye Mamlaka ya Spika ambapo yeye ndiye msimamizi wa masuala yote ndani ya Bunge. Kwa mujibu wa Kanuni, Wabunge wanapaswa kuheshimu uamuzi wa Kiti kuhusu suala lolote linalohusu utaratibu.

Mheshimiwa Spika, kumbukumbu Rasmi za Bunge zinathibitisha kuwa, Mwenyekiti alitumia muda mwingi kuwasihi wabunge mara kadhaa kuketi, ili shughuli iliyokuwa imepangwa iendelee. Katika ukurasa wa 70, 71 na 72 Mheshimiwa Mwenyekiti ameonekana akimsihi Mheshimiwa Mdee kuketi hata hivyo alikaidi maelekezo ya kiti. Mheshimiwa Tundu Lissu ameonekana kupaza sauti na kuomba mwongozo bila utaratibu. Aidha Mhe. Lissu katika ukurasa wa 86 ameonekana akihamasisha wabunge wengine kusimama na kuomba mwongozo jambo ambalo haliruhusiwi kikanuni.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Mheshimiwa Ester Bulaya ametajwa na Mwenyekiti katika ukurasa wa 89 kuwa, alikuwa akiongea bila kufuata utaratibu hivyo kuathiri shughuli zilizokuwa mezani. Kwa namna hiyohiyo, Mheshimiwa Zitto Kabwe ameonekana katika ukurasa wa 63, 64, 65 na 66 wa Hansard akibishana na Kiti na kukaidi maelekezo ya kumtaka aketi ambayo Mwenyekiti aliyatoa.

4.23 Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa 90 Mwenyekiti aliwasihi wabunge kutulia kama ifuatavyo

Mwenyekiti: Waheshimiwa Wabunge, sasa naagiza tuendelee na shughuli hii. Kama mnaona hakuna haja mna option ya kufanya, naendelea, Mheshimiwa Bashungwa. (Hapa baadhi ya waheshimiwa Wabunge waliendelea kuzungumza bila mpangilio”.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo ya baadhi ya Wabunge kuzungumza bila kuruhusiwa, Mwenyekiti alizungumza ifuatavyo: nukuu:

MWENYEKITI: Nimesimama tena kwa mara ya tatu, naomba mketi.

(Hapa Waheshimiwa Wabunge Kadhaa waliendelea kuomba mwongozo)

MWENYEKITI: Mketi.

Mheshimiwa Spika, mtiririko wa Mazungumzo yote katika ukurasa wa 90, 91 na 92 unaonesha vitendo vya kutotii maelekezo ya kiti na kuzungumza bila mpangilio. Katika ukurasa wa 92 Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya kuona vurugu zimezidi aliwataja baadhi ya Wabunge kuwa ndio walikuwa vinara wa Vurugu. Wabunge hao ni Mhe. Tundu Lissu, Mhe. Godbless Lema, Mhe. Pauline Gekul, na Mhe. Ester Bulaya. ”

Mheshimiwa Spika, kutokana na ufafanuzi huu, Kamati imewakuta na hatia ya kudharau Mamlaka ya Spika Waheshimiwa Wafuatao, Mhe. Godbless Lema, Mhe. Tundu Lissu, Mhe. Halima Mdee, Mhe. Pouline Gekul, Mhe. Ester Bulaya na Mhe. Zitto Kabwe.

Mheshimiwa Spika, aidha, Mhe. Godless Lema (Mb) alionesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu na dharau kubwa kwa Mamlaka ya Spika kwa kuvua koti na tai ikiwa ni ishara ya kujiandaa kupigana jambo ambalo halitegemewi kufanywa na kiongozi wa hadhi ya Mbunge kama Mhe. Godbless Lema. Amenukuliwa katika ukurasa wa 92 wa kumbukumbu rasmi za Bunge akisema maneno yafuatayo. Nukuu:

“MHE. GODBLESS J. LEMA: Mimi wataniua hapa tunagombania haki

(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabungee waliendelea kuzungumza bila ya mpangilio)

Mheshimiwa Spika, kauli iliyotolewa na Mhe. Godbless Lema ya kuwa”hapa wataniua, tunagombania haki” ni ishara ya kutaka kugombana ndani ya Bunge kitu ambacho hakiruhusiwi na ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kwa Msamlaka ya Spika na hakipaswi kuvumiliwa kwa vyovyote vile na Bunge letu Tukufu na watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuhitimisha kufanya uchambuzi wa shahidi mmoja baada ya mwingine, sasa naomba kujielekeza katika suala moja muhimu sana ambalo ulielekeza Kamati ilifanyie kazi. Katika maelekezo yako, uliitaka Kamati kufanya uchunguzi wa Mwenendo mzima wa Kambi ya Upinzani Bungeni katika tukio la tarehe 27 Januari, 2016.

Mheshimiwa Spika, tukio la tarehe 27 Januari, 2016 lilileta fedheha kubwa sana katika Bunge Letu Tukufu kwa wananchi wanaofuatilia shughuli zinazofanywa na wawakilishi wao na taifa kwa ujumla. Miongoni mwa mila na desturi zilizojengeka katika taifa letu ni pamoja na kujadiliana kwa hoja bila kujali tofauti zetu tulizonazo za kiitikadi, dini, umri au rangi. Mwalimu Julias Nyerere alitufundisha kujenga hoja na sio kupiga kelele (ague don’t shout). Ustaraabu huo umetujengea heshima kubwa mbele ya mataifa mbalimbali duniani.

Mheshimiwa Spika, Bunge ni mahali ambapo hoja kuhusu matatizo ya wananchi zinajadiliwa na kuamuliwa. Bunge ndicho chombo ambacho ni chemchem ya fikra za kulisaidia taifa letu na zinapaswa kutolewa ili taifa liweze kupiga hatua katika kujiletea maendeleo. Ili ndoto hii iweze kutimia ni lazima kuwe na staha na kuheshimiana ndani na nje ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 27Januari, 2016 Wabunge wa Upinzani waliokuwepo Bungeni baada ya amri ya Mwenyekiti ya kuwatoa nje wabunge wanne, hawakuonesha kusikitishwa natukio hilo badala yake waliunga mkono vurugu na hivyo kufanya kazi ya kuwatoa nje ya ukumbi kuwa ngumu hivyo kulazimu Mpambe wa Bunge kuingiza askari wengi ukumbini ili kuwatoa wabunge hao.

Mheshimiwa Spika, Kamati imesikitishwa sana na vitendo vya vurugu na uvunjwaji wa Kanuni za majadiliano Bungeni uliofanywa na Wabunge wa Upinzani waliokuwepo na kuhusika katika vurugu hizo zilizopelekea shughuli za Bunge zilizokuwa zimepangwa kwa siku hiyo kuahirishwa na Wabunge wote wa Kambi ya Upinzani waliokuwepo siku hiyo kutolewa nje ya Ukumbi wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, Kamati inatoa onyo kali kwa wabunge wote wa Kambi ya Upinzani Bungeni waliokuwepo na kuhusika katika kufanya vurugu na kwamba Mbunge yeyote aliyehusika na vurugu hizo, iwapo atarudia kutenda makosa hayo, atachukuliwa kuwa amerudia kutenda makosa hayo na ataadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 74(3)(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

MAONI NA MAPENDEKEZO YA JUMLA YA KAMATI KUHUSU UBORESHAJI WA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA BUNGE

Mheshimiwa Spika, pamoja na kushughulikia suala la baadhi ya Wabunge waliohusika kufanya fujo siku ya tarehe 27 Januari, 2016, Kamati imebaini masuala mbalimbali ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na Bunge lako Tukufu ili kuhakikisha kuwa utaratibu bora wa utekelezaji wa majukumu ya kibunge unazingatiwa. Masuala hayo ni kama yafuatayo:-

Kwa kuwa tangu kuanza kwa Bunge la Kumi na Moja imejengeka tabia ya kuzomea zomea wakati shughuli za Bunge zinapokuwa zinaendelea Bungeni na tabia hiyo inaelekea kuwa ya kawaida na kwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Wabunge wa Bunge la Kumi na Moja wapya, Kamati inapendekeza Bunge liandae mafunzo ya kutosha kwa wabunge wote kuhusu matumizi na uzingatiaji sahihi wa Kanuni za Kudumu za Bunge na hasa kanuni za majadiliano ndani ya Bunge. Mafunzo hayo yatasaidia kuondokana na changamoto hiyo na kudumisha hadhi na heshima ya Bunge letu tukufu.

Kwa kuwa imekuwa tabia ya kila siku kuomba mwongozo kwa kutumia Kanuni ya 68(7), Kamati inapendekeza Bunge liangalie matumizi sahihi ya neno”Mwongozo wa Spika” ili kuhakikisha kuwa malengo ya utungwaji wa Kanuni hiyo yanazingatiwa. Kwa kuwa katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia kuwepo kwa changamoto ya mienendo ya baadhi ya Wabunge ndani na nje ya Bunge ambayo imekuwa hairidhishi, Kamati inaona upo umuhimu mkubwa kwa Bunge kutunga Kanuni za Maadili kwa Wabunge wote kama kifungu cha 12A Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kinavyoelekeza ili kuweza kudhibiti nidhamu kwa Wabunge kwa lengo la kuhakikisha kuwa heshima na hadhi ya Bunge inadumishwa.

(d) Kwa kuwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hawazingatii Kanuni wanapokuwa Bunge hivyo kuifanya kazi ya Kiti kuwa ngumu na Kwa Kuwa Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananch kwa mujibu wa Ibara ya 62 na 63, hivyo basi, Kamati inatoa rai kwa Wabunge wote kuheshimu kiti pamoja na Kanuni tulizojiwekea ili kulinda hadhi na heshima ya Bunge letu.

HITIMISHO Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii kuwasilisha maoni ya Kamati kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na napenda nitumie nafasi hii tena kukupongeza kwa dhati kwa jinsi unavyoliongoza Bunge hili ambalo ni chombo cha uwakilishi wa Wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ili kuhakikisha kuwa ustawi wa wananchi unakuwa ndio kipaumbele cha kwanza.

Mheshimiwa Spika, kipekee, nawashukuru Wajumbe wote wa Kamati, kwa kazi nzuri ya kujadili na kuchambua kwa umakini mkubwa shauri hili kwani katika kutekeleza jukumu hili walizingatia utaifa mbele na misingi ya haki. Kwa heshima naomba niwatambue kwa majina kama ifuatavyo:-

Mhe. Kapt(Mst), George H. Mkuchika(Mb) - M/kiti

Mhe. Almas Maige, (Mb) - Makamu Mwenyekiti

Mhe. Rashid Ali Abdallah,(Mb)…………..Mjumbe

Mhe. Amina Nassoro Makilagi,(Mb)…….Mjumbe

Mhe. Dkt. Christine G. Ishengoma,(Mb)……Mjumbe

Mhe. Othman Omar Haji,(Mb)……………Mjumbe

Mhe. Rose Kamili Sukum,(Mb)………………Mjumbe

Mhe. George Malima Lubeleje,(Mb)………Mjumbe

Mhe. Dkt. Suleiman Ally Yussuf,(Mb)……….Mjumbe Mhe. Susan Anselm Lyimo,(Mb) ……………Mjumbe

Mhe. Tunza Issa Malapo,(Mb)………………Mjumbe

Mhe. Dkt. Hadji Hussein Mponda,( Mb)……Mjumbe

Mhe. Najma Murtaza Giga,(Mb)……………Mjumbe

Mhe. Hafidh Ali Tahir, (Mb)…………………..Mjumbe

Mhe. Innocent Sebba Bilakwate, (Mb)……Mjumbe

Aidha, napenda kumshukuru kwa dhati Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas D. Kashililah, kwa kuisaidia Kamati kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Kipekee, nawashukuru Ndugu Pius T. Mboya, Kaimu Mshauri Mkuu wa Bunge wa Mambo ya Sheria, Ndugu Prudence Rweyongeza, Naibu Mshauri Mkuu wa Bunge wa Mambo ya Sheria Sehemu ya Huduma ya Sheria kwa ushauri wa Kisheria walioutoa katika kuisaidia kamati. Aidha napenda kuwashukuru ndugu Matamus Fungo, Maria Mdulugu, Lweli Lupondo na Editruda Kilapilo kwa kuratibu vyema kazi za Kamati na kuhakikisha kuwa Taarifa hii inakamilika mapema.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ni matarajio yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge wataipokea na kwa kauli moja wataikubali hoja iliyopo mbele yetu ya matokeo ya taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ya uchunguzi wa vitendo vya baadhi ya Wabunge waliohusika kufanya vurugu Bungeni na kudharau Mamlaka ya Spika tarehe 27 Januari, 2016 ili kuimarisha nidhamu ndani ya Bunge letu na kuhakikisha kuwa Kanuni za Majadiliano Bungeni, zinaheshimiwa na kuzingatiwa na Wabunge wote.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Kapt. (Mst) George H. Mkuchika, (Mb.)

MWENYEKITI

KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE

30 MEI, 2016


======================

AZIMIO LA BUNGE KUHUSU ADHABU KWA WABUNGE WALIOFANYA VURUGU BUNGENI NA KUDHARAU MAMLAKA YA SPIKA KATIKA KIKAO CHA PILI CHA MKUTANOWA PILI WA BUNGETAREHE 27 JANUARI, 2016

[Limetolewa chini ya Kifungu cha 30A (1) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 74 (4) na (6)]

Kwa kuwa, Bunge letu linaongozwa kwa Mujibu wa Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge ambazo tulizitunga sisi wenyewe kwa ajili ya kutuongoza katika kutekeleza shughuli za Bunge.

Na Kwa kuwa, Sheria na Kanuni hizo zimeweka masharti kuhusu utaratibu unatakiwa kufuatwa katika majadiliano Bungeni na kwamba katika majadiliano hayo, Wabunge wanapaswa kuheshimu na kutii mamlaka ya Spika.

Na Kwa kuwa, Siku ya tarehe 27 Januari, 2016 baadhi ya Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni walifanyavurugu na kudharau mamlaka ya Spika.

Na Kwa kuwa,Mheshimiwa Spika alipeleka suala la baadhi ya wabunge hao kufanya vurugu na kudharau mamlaka ya Spika kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kuwataja majina Wabunge wafuatao:-
i) Mhe. Godbless J. Lema, (Mb)
ii) Mhe. Pauline Gekul, (Mb)
iii) Mhe. Ester A. Bulaya(Mb);na
iv) Mhe.Tundu Antiphas Mughwai Lissu,(Mb)

Na kwa kuwa pia,Spika aliwasilisha majina mengine matatu siku ya tarehe 10 Machi, 2016 ili Kamati iweze kufanya uchunguzi kuhusu ushiriki wao katika vurugu zilizotokea siku tajwa hapo juu.

Majina ya Wabunge walioongezwa ni hawa wafuatao:-
(i) Mhe. Kabwe Zuberi. Ruyagwa Zitto, (Mb)
(ii) Mhe.John W. Heche (Mb), na
(iii) Mhe. Halima James Mdee, (Mb)

Na Kwa Kuwa, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilikaa kati ya tarehe 07Machi, 2016 hadi tarehe 12 Machi, 2016 Jijini Dar es salaam kabla ya kuahirishwa kwa muda kutokana na wajumbe wa Kamati hii kuwa wajumbe wa Kamati za kisekta ambazo Wajumbe walitakiwa kuhudhuria vikao vya Kamati. Kamati ilirejea tena tarehe 16 Mei, 2016 hadi tarehe 29 Mei, 2016 na kufanya uchunguzi wa shauri hili.

Kamati iliweza kubaini kuwa, Wabunge wafuatao wamevunja masharti ya Kifungu cha 24(c),(d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 72 (1) 68 (10),60(2)&(12) na 74 (1)(a) na (b) kwa kusimama na kuendelea kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi, kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau Mamlaka ya Spika.
(i) Mhe. Tundu Lissu, (Mb)
(ii) Mhe. Halima Mdee, (Mb)
(iii) Mhe. Pauline Gekul, (Mb) na
(iv) Mhe. Ester Bulaya,(Mb)

Na kwa kuwa,Mhe. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto(Mb), alivunja masharti ya Kifungu cha 24(c),(d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 60(2)na (12), 74(1) (a) na (b) na kwa kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau mamlaka ya Spika
Na kwa KuwaMhe. Godbless Lema(Mb) alivunja masharti ya Kifungu cha 24(c), (d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296pamoja na Kanuni ya 74(1)(a) na (b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kudharau Mamlaka ya Spika.

Na kwa kuwa,Mhe. John Heche(Mb) alivunja Kanuni ya 72(1) na 68(10) ya Kanuni za Bunge kwa kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo lilikwishatolewa Mwongozo.

Na Kwa Kuwa, vitendo hivyo visivyo na tija, vilivuruga shughuli za Bunge zilizokuwa zikiendelea na kuathiri heshima ya Bunge Mbele ya Umma wa Watanzania jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:
(a) Wabunge wafuatao:
(i) Mhe. Ester A. Bulaya, (Mb) na
(ii) Mhe. Tundu A. Mughwai Lissu(Mb)

wasihudhurie vikao vyote vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyobaki kuanzia tarehe 30 Mei, 2016pamoja na vikao vyote vya Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na Moja kwa kuwa walipatikana na makosa ya ukiukwaji wa Kanuni na kuonyesha dharau kubwa kwa Mamlaka ya Spika na pia walihusika kwa kiasi kikubwa kuchochea vurugu zilizotokea siku ya tarehe 27 Januari, 2016.

Aidha, Bunge linaazimia kuwa:
(b) Wabunge wafuatao:
i) Mhe. Pauline Gekul (Mb)
ii) Mhe. Godbless Lema(Mb)
iii) Mhe. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto(Mb) na
iv) Mhe. Halima James Mdee(Mb)

Wasihudhurie vikao vyote vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyosalia kuanzia tarehe 30 Mei, 2016 kwa kuwa walifanya vitendo ambavyo ni vya utovu wa nidhamu na dharau kubwa kwa Mamlaka ya Spika. Vitendo hivyo vya vurugu walivyovifanyavilisababisha kuvurugika kwa Shughuli za Bunge.

Vilevile Bunge linaazimia kuwa:
(c) Mhe. John W. Heche (Mb)
Asihudhurie vikao Kumi mfululizo vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja kuanzia tarehe 30 Mei, 2016.Adhabu hiyo kwa Mhe. John Heche (Mb) imezingatia kwamba alipatikana na kosa moja na pia kwa kuwa alitoa ushirikiano kwa Kamati kwa kutii wito wa Kamati wa Kufika na analiju maswali yote kama yalivyoulizwa pamoja na kuheshimu vikao vya Kamati na Mwenyekiti aliyeongoza vikao hivyo.


KWA HIYO BASI, kwa mujibu wa Kifungu cha 30A (1) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 74 (4) na (6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalokutana katika Mkutano wa Tatu, linapokea na kukubali adhabu inayopendekezwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa Wabunge waliofanya vurugu siku ya tarehe 27 Januari, 2016 na linaazimia kupitisha mapendekezo ya adhabu kwa Wabunge husika.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na kutoa hoja.

Kapt.(Mst). George H. Mkuchika, Mb
MWENYEKITI KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE

30 Mei, 2016