May 27, 2016

TCRA: HATUTAWALIPA FIDIA WENYE SIMU FEKI NA WALA HATUTAONGEZA MUDA WA KUZIMA SIMU HIZOWakati siku ya kuzimwa kwa simu feki ikikaribia,Mamlaka ya MawasilianoTanzania(TCRA),imesema haina mpango wa kuongeza siku za kuzima simu hizo wala haitahusika kulipa fidia kwa watakaoathirika baada ya simu zao kuzimwa. 

Jana Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana CUF(JUVICUF),Mahamoud Mahinda,aliitaka serikali kubeba mzigo wa kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa kuruhusu uingizaji wa simu feki nchini.
Mahinda,alisema serikali ilishindwa kutimiza wajibu wa kuhakikisha simu hizo haziingizwi nchini,hivyo inapaswa kuwajibika,na kuwaacha wananchi kununua simu feki siku za nyuma bila ya kudhibiti uingizwaji wake nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi,mara baada ya semina ya kwa umma juu ya ufahamu wa mfumo wa rajisi wa namba za utambulishi wa simu za kiganjani mkoani Geita,Meneja wa TCRA nchini Innocent Mungy alisema mamlaka hiyo haina mpango wa kuwalipa fidia wenye simu feki.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa TCRA James Kilaba,Mungy, alisema ifikapo Juni 16 simu hizo zitafungwa.

"Kipindi cha Mpito(Transition period) cha kuelimisha umma pamoja na zoezi la wateja kuhakiki simu walizo nazo au wakati wanataka kununua simu mpya lilianza mwezi disemba mwaka jana wakati huo mfumo ulipozinduliwa na itamalizika Juni 16"alisema Mungy.
 

Alisema,ikifika saa 6 usiku Juni 16,mwaka huu simu hizo zitafungwa,na wala TCRA haikusudii kuongeza muda wa kuzima simu hizo ,na mtu atayekaa na simu feki akikamatwa atachukuliwa hatua za kisheria.