May 21, 2016

MWANAFUNZI MBARONI KWA KUWATUKANA RAIS WA ZANZIBAR NA MKUU WA MAJESHIJeshi la polisi mkoani Arusha linamshikilia mwanafunzi wa Mwaka wa tatu wa chuo cha maendeleo ya jamii Tengeru aliyejulikana kwa jina la Harold Mmbando (23) mkazi wa Arusha kwa kosa la kutoa taarifa za uchochezi dhidi ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na Mkuu wa majeshi Davis Mwamunyange pamoja na kusambaza ujumbe wa maneno makali juu ya viongozi hao.

Akiongelea tukio hilo kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Charles Mkumbo alisema kuwa tukio hilo lilitokea May 17 mwaka huu majira ya saa 09:00 asubuhi.

Alisema kuwa mwanafunzi huyo alitoa taarifa za uchochezi kuhusu mkuu wa majeshi ambapo alimtaka mkuu huyo wa majeshi kupindua nchi na kusema kuwa haiwezekani viongozi wote wawe nje ya nchi huku hakuna kiongozi aliyepewa mamlaka ya kukikaimu kiti.

Mtuhumiwa huyo aliandika maneno haya "Mwamunyange pindua nchi haiwezekani wote wawe nje halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti"

Aidha aliongeza kuwa  ”Dr. Shein akiuawa kama Karume sitashangaa wala kustuka naomba mungu mauaji ya kisiasa yaliyotokea Zanzibar yawe kwa viongozi wa kisasa hasa watawala na sio wananchi wa kawaida"