May 10, 2016

KATIBU WA TUME YA UTUMISHI NA NIDHAMU YA WALIMU(TSD) AJINYONGAKatibu wa Tume ya Utumishi na Nidhamu ya Walimu (TSD ) Wilaya ya Muleba, Manase Mkumbo amekutwa amefariki dunia kwa kujinyonga shambani mwake katika Kijiji cha Kyamyorwa wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Francis Isack amesema Mkumbo alijinyonga usiku kuamkia leo.

Amesema kabla ya tukio hilo alituma ujumbe wa maandishi kwa simu akimjulisha mwanae aliye masomoni kuwa amekata tamaa na maisha.

Isack amesema Mkumbo aliondoka Muleba kwenda kukagua mashamba yake kijijini ambako aliandika ujumbe huo na kununua kamba ya katani na kujinyonga.

Ujumbe huo ulipomfikia mtoto wake aliutuma tena nyumbani katika Kitongoji cha Bugombe wilayani Muleba ndipo wakaanza kufuatilia kwa kuwa alikuwa amewaaga kuwa anaelekea shambani ambako walikuta mwili wake umetundikwa.

“Inasikitisha mtu alibakiza mwaka mmoja astaafu na kupata mafao yake lakini anaamua kujiondoa na kuacha hasara na simanzi kwa familia,” amesema Isack.

Amesema taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kwao mkoani Singida zinaendelea.

Chanzo: Mwananchi