April 9, 2016

WAZIRI MKUU: HALMASHAURI AMBAZO ZITAKUSANYA MAPATO CHINI YA 80% NITAZIFUTAWaziri mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh.Majaliwa Kassim Majaliwa amesema Halmashauri yeyote itakayoshindwa kukusanya mapato juu ya asilimia 80 kuanzia hivi sasa serikali itaifuta huku akiendelea kutahadharisha kuwa vita dhidi ya rushwa na ufisadi ni ya kudumu ndani ya serikali ya awamu ya tano.

Mh. Waziri Mkuu Kasim Majaliwa ameyasema hayo katika wa mkutano mkuu wa jumuiya ya tawala za mitaa Tanzania ALAT ambapo amesema moja ya changamoto inayoikosesha serikali mapato ni rushwa na kuwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele kuchukia rushwa na ufisadi unaoligharimu Taifa na kuhakikisha mapato ya kwenye kila halmashauri yanaongezeka kwa kutumia mfumo wa ukusanyaji kodi na ushuru wa kielektronoki.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jafo anasema kuwa endapo viongozi wa halmashauri watasimamia vyema maeneo yao kuna kila sababu ya Tanzania kusonga mbele katika nyanja ya maendeleo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa ALAT Taifa Gullam Hafidh Muqaddam amesema ameitaka serikali kupeleka ruzuku katika halmashauri kama inavyoainishwa kwenye bajeti ili kuharakisha maendeleo na kuondoa misuguano baina ya watendaji wa halmashauri na wananchi.