April 15, 2016

SUDANI YA KUSINI YAJIUNGA RASMI EACSudan Kusini sasa ni mwanachama mpya wa jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya Rais wa nchi hiyo Salva Kiir kusaini mkataba wa kujiunga rasmi na jumuiya hiyo.

Rais Kiir ametia saini mkataba huo jijini Dar es Salaam mbele ya mwenyeji wake Rais wa Tanzania John Magufuli ambaye kwa sasa ndiye Mwenyeketi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema kujiunga kwa nchi yake na jumuiya hiyo kumemfanya kujihisi kuwa kwenye jumuiya sahihi.

“Ninaposimama hapa leo hii, moyo wangu umejawa na furaha na hali ya kuridhishwa kuwa sehemu ya jumuiya hii kuu. Kwa ujasiri kabisa ninaweza kusema hatimaye Sudan Kusini imepata mahala sahihi katika jumuiya,” alisema Rais Kiir.

Viongozi wa nchi za jumuiya hiyo waliidhinisha kukubaliwa kwa Sudan Kusini kujiunga na jumuiya hiyo kwenye mkutano mkuu uliofanyika mjini Arusha mwezi uliopita.