April 7, 2016

SERIKALI YABAINI WATUMISHI HEWA 1855 NCHINIWaziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa George Simbachawene amewataka wakuu wa mikoa ambayo imekutwa na watumishi hewa kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi waliohusika kulipa na kupokea mishahara hewa. 

Akizungumza na wakuu hao wa mikoa mara baada ya kukabidhiwa ripoti hizo, Waziri Simbachawene aliwataka viongozi hao kuhakikisha kuwa wanawakamata watumishi hao kwa makosa waliyobainika nayo na hatua stahiki.  

"Wananchi wanataka kusikia hawa waliokuwa wanaiibia serikali wamechukuliwa hatua gani mara baada ya kutangazwa badala ya kuishia kuwatangaza kuwa ni watumishi hewa na wanalipwa mishahara," alisema. 

Jumla ya watumishi hewa 1855 wamebainika kuwepo katika mikoa mbalimbali nchini huku mkoa wa Mwanza ukiwa na watumishi hewa 334, Arusha 270 na Sungida 202.

Mikoa ya Mwanza, Arusha na Singida inaongoza kwa kuwa na watumishi hewa wengi. Kwa mujibu wa taarifa hizo kutoka kwa wakuu wa mikoa, watumishi waliobainika kuwa ni hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara ni walimu na madaktari ambao ni marehemu na wastaafu.  

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais John Magufuli, kuwaagiza wakuu hao wa mikoa kuwasilisha ripoti ya watumishi hewa ambayo waliikabidhi kwa Simbachawene jana jijini Dar es Salaam kabla ya kuiwasilisha kwa Waziri wa Utumishi na kujumilisha na ripoti za sekta zote nchini na hatimaye kumfikishia Rais. 

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema jumla ya watumishi hewa 334 walibainika kwenye mkoa huo hususani katika Halmashauri ya jiji la Mwanza ambalo lina watumishi hewa 72 pekee.  

Katika mkoa wa Arusha jumla ya watumishi hewa 270 walibainika katika kipindi cha wiki mbili na kusababisha upotevu wa Sh. bilioni 1.188 kwa mwezi March pekee.Katika mkoa wa Singida jumla ya watumishi hewa 202 walibainika na mkoa wa Kigoma wenye watumishi hewa 171 ambao wamesababisha hasara ya Sh. milioni 114.6 kwa mwezi.  

Mikoa mingine ni Kilimanjaro wenye jumla ya watumishi hewa 111 ambao waliolipwa Sh. milioni 281.4 kwa mwezi mmoja na Dodoma watumishi hewa 101 waliolipwa Sh. bilioni 297 kwa muda wa miezi sita. 

Pia katika mkoa wa Morogoro watumishi hewa waliobainika ni 122 ambao walilipwa Sh. milioni 450.79 kwa mwezi March pekee na mkoa wa Mara watumishi hewa 94 ambao walilipwa Sh. milioni 121.1 kwa mwezi mmoja.  

Mkoa wa Mbeya ambao umeungana na mkoa mpya wa Songwe ulibainika kuwa na watumishi hewa 98 ambao walilipwa mishahara kiasi cha Sh. milioni 459.6. 

Katika jiji la Dar es Salaam watumishi hewa waliobainika ni 73 ambao wamelipwa Sh. milioni 379 kwa mwezi mmoja.  

Mikoa mingine ni mkoa wa Pwani uliobainika kuwa na watumishi hewa 150, Ruvuma watumishi hewa 37 ambao walilipwa Sh. milioni 58. 4, Njombe watumishi hewa 34 ambao walilipwa Sh. Milioni 20.107 na mkoa wa Rukwa wenye watumishi hewa 18 waliolipwa mishahara Sh. Milioni 55.64. 

Watumishi wengine hewa walibainika katika mikoa ya Simiyu 33 ambao walilipwa Sh. Milioni 320.993 , Tabora jumla ya watumishi hewa 48 ambao walilipwa Sh. Milioni 118, Tanga watumishi hewa 24 na Lindi watumishi 57 waliolipwa Sh. Milioni 36.  

Mikoa mingine ni Katavi wenye watumishi hewa 21 ambao walilipwa Sh. milioni 120 kwa miezi sita, kagera 14 ambao walilipwa Sh. milioni 49. 147 kwa mwezi, Geita wenye watumishi hewa nane na Manyara wenye watumishi hewa watano. 

Aidha katika mkoa wa Shinyanga haukubainika kuwa na watumishi hewa kutokana na malengo waliyokuwa wamejiwekea tangu mwaka 2014, ikiwamo kukagua idadi ya watumishi walioko kazini na wanaotakiwa kulipwa mishahara kila mwezi.  

Pia katika ripoti hizo walibainika watumishi watoro ambao walikuwa wakiendelea kulipwa mishahara licha ya kutokuwepo kazini kwa muda mrefu. 

Katika mkoa wa Dodoma jumla ya watumishi watoro 38 walibainika, Iringa 145 na Kagera watumishi 248 ambao pia wanaendelea kuchunguzwa.  

Mkoa wa Manyara jumla ya watumishi watoro 50, Mtwara watumishi 285 watoro, Mwanza watumishi watoro 205, Pwani watumishi watoro 50 , Rukwa watumishi watoro 139 na Simiyu watumishi watoro 62. 

Mkoa wa Singida watumishi watoro 29 na Tanga jumla ya watumishi watoro 502. Watumishi hao watoro ni wale walioacha kazi lakini wamekuwa wakiendelea kulipwa mishahara na wengine walio kwenye matatizo ya kiutumishi.