April 15, 2016

NAPE: MADIWANI WAZINGATIE VIWANJA VYA MICHEZO KATIKA KILA MPANGO MJI WA MAKAZI YA WATUWaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye leo ameendelea na ziara yake katika mkoa wa Mara na Shinyanga ambapo alikutana na Watumishi na wadau walio chini ya Wizara yake. 

Waziri Nape alipokea taarifa zaSerikali pamoja na maoni ya wadau mbali mbali ambapo aliwapongeza kwa kuwa na maoni mazuri na kusisitiza Wizara yake itakuwa karibu nao na kufanya ziara za mara kwa mara katika kuhakikisha mambo waliyopanga yanafanikiwa. 

Waziri Nape aligusia mambo mbali mbali ya msingi wakati akiongea na washika dau waliokuwa chini ya wizara yake na kusisitiza kuwa Madiwani wanaoshiriki katika mipango mji wanatakiwa kuzingatia kutenga viwanja vya michezo kwa watoto wa eneo husika pia alishauri mikoa kuanzisha vituo vya utamaduni wa mkoa ambavyo vitakuwa vyanzo vya kutunza utamaduni lakini pia sehemu ya kuvutia utalii akitolea mfano kituo cha Bujora mkoani Mwanza. 

Mhe. Nape pia aliwataka Makatibu Tawala za Mikoa  wajenge utamaduni wa kukutana na vyama vya michezo kwani wao ni walezi muhimu wa vyama hivyo.