March 30, 2016

WAZIRI MUHONGO AWATAKA WAKANDARASI WA REA KUKAMILISHA USAMBAZAJI UMEMEWaziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) awamu ya pili kufanya kazi kwa kasi zaidi ili umeme uweze kuwafikia walengwa kabla ya mwezi Juni mwaka huu. 

Akizungumza na watendaji kutoka kampuni ya CCC International Nigeria Limited, inayosambaza umeme katika mkoa wa Manyara, Profesa Muhongo alisema kuwa hajaridhishwa na kasi ya kampuni hiyo katika utekelezaji wa miradi ya umeme katika wilaya ya Simanjiro ambapo hakuna wateja waliounganishiwa umeme. 

Pia, Profesa Muhongo amelitaka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kufanya kazi kwa karibu na wakandarasi hao katika kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kukamilisha miradi hiyo kwa wakati. 

Aliwataka mameneja wa TANESCO kuongeza juhudi katika kazi zao ikiwa ni pamoja na makusanyo, utatuaji wa changamoto na uunganishaji wa umeme kwa wateja, na kusisitiza kuwa meneja atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake ataondolewa katika nafasi yake. 

Awali, akielezea changamoto katika utekelezaji wa miradi ya umeme meneja mradi kutoka CCC International Nigeria Limited.Zhang Jiangaang, alieleza kuwa wamekuwa wakiibiwa vifaa vyao vya kazi kutokana na kuwepo kwa usalama mdogo hivyo kupelekea kutokamilisha mradi kwa wakati kutokana na hasara wanayoipata.