March 10, 2016

WAFANYABIASHARA WAGOMA KUSHUSHA BEI YA SUKARILicha ya Bodi ya Sukari Tanzania kutangaza bei elekezi ya bidhaa hiyo kuwa ni Sh1,800 kwa Dar es Salaam, maeneo mbalimbali bado inauzwa kwa Sh2,200.

Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Henry Semwanza alisema bei hiyo itatumika kwa maduka yote ya rejareja na wafanyabiashara wanatakiwa kuizingatia pamoja na kuendelea kusambaza sukari kwa wingi.

Mfanyabiashara wa duka la jumla eneo la Manzese, Alex Brayton alisema alikuwa akiuza sukari kwa bei ya rejareja Sh2,200 na kwamba sababu kubwa ni kwamba sukari inayozalishwa viwandani haionekani wala haitoshelezi hivyo wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wanawauzia kwa bei ya juu.

“Suala la kushusha sukari hadi kufikia Sh1,800 kwa bei elekezi halitawezekana kwa kuwa bei ya jumla ya kilo moja tunauziwa Sh2,000 hivyo tunalazimika kuuza Sh2,200 ili kilo moja tupate faida ya Sh200,” alisema Brayton. Mfanyabiashara mwingine wa duka la jumla Magomeni, Idrisa Abraham aliyekuwa akiuza mfuko wa sukari wa kilo 50 kwa Sh98,000 na wa kilo 25 kwa Sh48,000, alisema kabla ya kutoa bei elekezi, Serikali ilitakiwa kufanya utafiti ili kubaini sababu ya kutoonekana kwa bidhaa hiyo na kukutana na wafanyabiashara wanaosambaza na wa maduka ya jumla ili kujua kwa nini sukari ya Tanzania haionekani na kinachoifanya kupanda “...nina imani wangebaini kitu, kinachonishangaza sukari iliyokuwa inatoka Malawi na Brazil ilikuwa inauzwa kwa bei nafuu sana na ilikuwa inalipiwa kodi kwa nini ya Tanzania iwe bei juu?”

Pia, alisema kuna janja imeanza kutumika kwa kuhifadhi sukari hiyo kwenye mifuko ya kampuni za viwanda vya ndani, jambo ambalo ni hatari zaidi.