March 29, 2016

MKAGUZI WA HESABU ZA SERIKALI(CAG) AKABIDHI RIPOTI YA 2014/2015 IKULU


Rais Dkt. John Pombe Magufuli amepokea taarifa ya ukaguzi wa hesabu za serikali kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Assad, Ikulu Jijini Dar es salaam. 
 
Rais Magufuli amepokea taarifa hiyo yenye ripoti tano, ikiwa ni utaratibu wa kikatiba unaomtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, kukabidhi kwa Rais taarifa ya ukaguzi kabla ya mwisho wa mwezi Machi. 
 
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli ataikabidhi mbele ya bunge katika siku saba za mwanzo za kikao kijacho cha Bunge kitakachofanyika Mjini Dodoma. 
 
Rais Magufuli amempongeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali na timu yake kwa kuandaa taarifa hiyo, na ametoa wito kwa chombo hicho kuendelea kufanya kazi kwa uhuru na ufanisi, huku akiahidi kuwa serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha kazi zake.
 
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
28 Machi, 2016