December 7, 2015

WAFANYAKAZI HALMASHAURI YA HAI WASIMAMISHWA KWA UBADHILIFU WA TSHS MILIONI 512.3

Wafanyakazi 11 wa halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wakiwemo afisa utumishi wa wilaya, mchumi, mhasibu na afisa ugavi, afisa muuguzi na katibu wa afya wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za serikali zaidi ya shs. 512.3mil/= kati ya Julai na Juni mwaka huu.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Bw Saidi Mderu amesema, ukaguzi uliofanywa umejiridhisha kuwa katika siku tofauti watumishi hao walitumia nyaraka zilizonunua dawa hewa za hospitali, kuidhinisha malipo bila kibali cha murugenzi mtendaji, mweka hazina na baraza la madiwani ambalo ndilo lenye maamuzi ya mwisho.

Bw Mderu amewaambia waandishi wa habari kuwa, watumishi hao pia kwa nyakati tofauti katika kipindi hicho walitumia madaraka yao kuidhinisha matumizi ya shs. 404mil/= kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambazo hazikufanya kazi iliyokusudiwa, kujikopesha shs. 35mil/= kupitia benki ya CRDB na kutumia fedha za posho za kujikimu madaktari na wauguzi wa hospitali ya machame.

Mkurugenzi huyo amesema, watumishi hao wamesimamishwa kazi wakati uchunguzi ukiendelea ili wasipoteze nyaraka muhimu na baada ya hapo watachukuliwa hatua za kinidhamu na vyombo vya dola vichukue mkondo wake wa kuwafikisha mahakamani.