December 30, 2015

HALMASHAURI ZATAKIWA KUFUNGA MFUMO WA UKUSANYAJI MAPATO WA KIELEKTONIKI.



Naibu Waziri Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Seleman Said Jaffo ameziagiza halmashauri zote nchini ambazo bado zinaendelea kukusanya mapato yake bila ya kutumia mfumo wa kielektroniki ziwe zimefanya hivyo kabla ya tarehe 10 januari 2016.Akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi iliyopo Mkoani Dodoma, Mhe.Jaffo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha kuwa agizo lake linatekelezwa na kuhakikisha kuwa mfumo huo unafanyakazi katika idara zote muhimu za halmashauri ikiwemo Utawala, Afya na Maliasili.

Alisema kuwepo kwa mfumo huo kutazisaidia halmashauri kuboresha ukusanyaji wa mapato na hivyo kuwa na ongezeko la fedha kwa ajili ya kutoa huduma muhimu kwa wananchi hasa kuboresha upatikanaji wa dawa katika zahanati na vituo vya afya vya halmashauri za wilaya.Mhe.Jaffo aliongeza kuwa halmashauri zimekuwa zikikusanya mapato kidogo kutokana na kutokuwa na mfumo sahihi wa ukusanyaji mapato, na hivyo kuchangia mapato mengi kupotea mifukoni mwa watu. Pia Naibu Waziri alizungumzia kero inayowakabili watumishi wa chini ambao hawapati mrejesho pindi wanapohitaji huduma mbalimbali katika halmashauri zao.

Alisema kumekuwa na mtindo kwa wakuu wa idara na Maafisa wa Halmashauri kutoshughulikia malalamiko ya watumishi wa chini hasa madai ya likizo za watumishi na kutopandishwa vyeo katika madaraja mbalimbali, hivyo akatoa agizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kwa kushirikiana na Maafisa Utumishi kuhakikisha kuwa kero hiyo inashughulikiwa .

Alisema endapo ataulizwa swali bungeni kuhusu kero na malalamiko yanayohusu watumishi kutolipwa madai ya likizo na kutopandishwa madaraja kwa watumishi wa ngazi za chini hapo nitajua kuwa Mkurugenzi na Afisa Utumishi wa wa Halmashauri hiyo hatoshi katika nafasi yake ya utawala."Unakuta mtumishi anafuatilia madai yake muda mrefu bila kupewa mrejesho, na hivyo kukosa muda wa kuendelea na majukumu yake katika kituo chake cha kazi, nawaagiza maafisa utumishi kuhakikisha kuwa mnatoa mrejesho ili kuondoa kero hii" ,alisema Naibu Waziri

Kuhusu kutofanyika kwa Mikutano ya vijiji, Naibu Waziri alisema vijiji vingi nchini tangu kufanyike uchaguzi wa Serikali za Mitaa takribani mwaka mmoja uliopita havijafanya mikutano yake na matokeo yake wananchi wanachangishwa fedha lakini hawasomewi mapato na matumizi ya fedha hizo.

"Nina taarifa kuwa vijiji vingi havijafanya mikutano toka mwaka jana uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulipofanyika, hivyo naagiza kila kijiji kifanye mikutano yake ili wananchi wasomewe taarifa za mapato na matumizi" ,alisema

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Francis Mwonga alimshukuru Naibu Waziri kwa kuwatembelea na kuahidi kuyatekeleza maagizo mbalimbali yanayoihusu Wilaya yake.


Pia alisema kuwa changamoto kubwa inayoikabili wilaya hiyo mbali na tatizo la njaa, ni kukosekana kwa Maji ya uhakika.Mapema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi Bibi Rachel Chuwa alimweleza Naibu Waziri kuwa Halmashauri inakitegemea kisima kimoja cha maji ambacho kilichimbwa kutokana na fedha za wafadhili kutoka shirika la kimataifa la UNDP ambao walichangia shilingi milioni 230 ambapo serikali kuu iliahidi kuchangia shilingi milioni 680, ambapo licha ya kufuatilia fedha hizo lakini hadi sasa hawajaziopata.

Wilaya ya Bahi ilianzishwa mwaka 2007 baada ya kugawanywa iliyokuwa Wilaya ya Dodoma vijijini na mara kwa mara imekuwa ikikabiliwa na tatizo la njaa ambapo kwa mwaka huu wilaya ina upungufu wa tani 7000 za chakula na hadi sasa wamekwishapokea tani 300 cha chakula cha Msaada kutoka idara ya maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu.