November 23, 2015

RAIS DKT MAGUFULI AFUTA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA UHURU KUOKOA MAMILIONI YA FEDHA

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiongea na waandishi wa habari juu ya kufutwa kwa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Uhuru.

Rais John Pombe Magufuli amefutilia mbali sherehe za uhuru zinazoazimishwa kila mwaka. Sherehe hizi ni moja ya sherehe zinazotumia hela nyingi kwa ajili maonesho. Badala yake siku hiyo itatumika kwa kufanya usafi ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindu pindu.

Akitoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa vyombo vya habari Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue alisema "Rais amesema suala la kuwepo ugonjwa Kipindupindu halikubaliki, jambo hili limemkera sana, tunasherehekea miaka 54 ya uhuru lakini bado kipindupindu kinatusumbua sana. Amesema kama Watanzania lazima tulishughulikie. Haiwezekani akija mgeni kama Obama tunafanya usafi lakini akiondoka tunaendelea kuwa wachafu. Ameamua tarehe 9 December siku ya Uhuru hakutakuwa na sherehe yoyote badala yake watu wakasafishe maeneo yao”

"Amesema hakutakuwa na cha kwenda kwenye Gwaride, kila mkuu wa Mkoa au kiongozi yeyote wa eneo husika wanatakiwa waanze kuandaa vifaa vya usafi, itakuwa ni siku ya kufanya usafi ili kupunguza tatizo la uchafu..

Si kwamba tuna dharau siku hii bali tunaifanya kwa staili nyingine… Kuhusu pesa zitakazotumika siku hiyo Rais atatafuta kazi ya kuzifanyia, atazipeleka kwenye eneo jingine lenye tatizo".