September 11, 2015

WARIOBA AWASHANGAA MAWAZIRI WAKUU WENZAKE WASTAAFU

Waziri Mkuu Mstafu Jaji Joseph Sinde Warioba akihutubia wakazi wa Butiama ambapo aliwaeleza Magufuli anafaa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

WAZIRI Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, ameibuka katika kampeni za mgombea urais wa CCM Dk. John Magufuli na kusema kuwa anashangazwa na hatua ya mawaziri wakuu wenzake kuhama CCM na kudai hakuna kilichofanyika katika miaka 54 ya Uhuru.

Pamoja na hali hiyo amesema anajua wazi huenda hata wanachokifanya hawajui wajibu wao walipokuwa katika madaraka hayo kama washauri wakuu wa rais.alisema  sasa umefika wakati wa watu wanaomtumia kama dira Baba wa Taifa katika kampeni zao wajitafakari zaidi.

"Wengine katika kampeni zao wanatumia maneno ya Mwalimu kama wamechanganyikiwa. Huwezi kumtumia Mwalimu kama dira halafu unasema CCM haijafanya kitu, aliijenga Tanzania kwenye misingi na wote walimfuata wanapita kwenye misingi yake," alisema Jaji Warioba