September 22, 2015

UFAFANUZI KWA WALIOPOTEZA VITAMBULISHO VYA MPIGA KURA SOMA HAPA

Wakati zaidi ya robo tatu ya vifaa vinavyohitajika vikiwa vimewasili nchini, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema inaangalia namna ya kuwasaidia waliopoteza vitambulisho vyao kushiriki kupiga kura.

Kauli hiyo imetolewa baada ya idadi ya watu wanaotoa taarifa za kupotelewa na vitambulisho vya kupigia kura pamoja na wanaowasilisha vitambulisho vilivyookotwa kwa tume kuendelea kuongezeka kila siku licha ya uhakiki na uhamishaji wa taarifa za mpiga kura kumalizika mapema mwezi huu.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari wa NEC, Clarence Nanyaro amesema ni changamoto kwa tume kutokana na wingi wa watu wenye tatizo linalofanana na hatma yao ya kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba.

“Kwa wale waliojiandikisha na wakahakiki majina yao lakini wamepoteza vitambulisho tutaangalia namna ya kuishawishi tume itafute jinsi ya wao kushiriki kupiga kura kwasababu majina yao yapo kwenye datfari na yatarudishwa vituoni. Watakachotakiwa ni kuwa na ripoti ya upotevu huo kutoka polisi (Loss report),” amesema Nanyaro. Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) cha tume hiyo kinaendelea na kupakia taarifa za watu wote waliojiandikisha na Nanyaro amewatoa shaka wale ambao mpaka sasa wanaambiwa hawaonekani kwenye kumbukumbu.

Nanyaro amewataka wawe na uhakika wa kushiriki uchaguzi na kubainisha: “Kuna wale ambao wakihakiki taarifa zao kwa njia ya simu wanaambiwa hawatambuliki. Wasiwe na wasiwasi. Kazi ya kuingiza majina yote kwenye mtandao inaendelea na baada ya muda mambo yatakuwa sawia. Kama wanavitambulisho, inatosha kuwatambua hivyo wawe na
subira,’ ameongeza.