September 6, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Ndugu Thadeo Marko Mwenempazi kuwa Mshauri wa Rais Masuala ya Sheria. Uteuzi wa Ndugu Mwenempazi umeanza tokea Jumatatu ya Agosti 24, mwaka huu, 2015.

Taarifa iliyotolewa Ijumaa, Septemba 4, 2015 mjini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue imesema kuwa kabla ya uteuzi wake, Ndugu Mwenempazi alikuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkoa wa Dar es Salaam.

Ndugu Mwenempazi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Sirilius Matupa ambaye karibuni aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
04 Septemba, 2015