September 12, 2015

SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO YAANZA KUWATAFUNA WATU, WATU WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Watu wawili, Patrick Natala na Maxmillian Msacky  wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 10 yakiwamo ya kughushi, kutengeneza tovuti feki na mifumo ya mtandao kwa kutumia majina ya  Taasisi, viongozi na wanasiasa.

Akiwasomea hati ya mashtaka leo Wakili wa Serikali, Theophil Mutakyawa akishirikiana na Wakili Mwandamizi Mkuu wa TCRA, Johannes Kalungura walidai kuwa washtakiwa hao
walitengeneza tovuti feki kwa kutumia majina ya Taasisi ya Jakaya Kikwete Foundation (Ikulu), TCRA Foundation, Akiba Saccos Social Company, Social Credit and Loans Company, Ridhiwani Social Company, Hisa Tanzania, Zitto Kabwe Foundation, Vicoba Tanzania na  Wekeza Fund.

Mutakyawa amedai kuwa washtakiwa hao wametengeneza tovuti hizo feki kati ya Januari na Aprili 2014 jijini Dar es Salaam  kinyume na kifungu cha 122 (b) cha sheria ya Kielektoliniki na Mawasiliano ya Posta namba 3 ya 2010. Mbali na mashtaka hayo, Mshtakiwa Msacky yeye anadaiwa kuwa kati ya 2006 na 2024 kwa njia ya udanganyifu alighushi cheti cha Sekondari  namba 0421130 chenye indexi namba S 0260-0001.

Iliendelea kudaiwa kuwa  kati ya 2005 na 2014 mshtakiwa huyo alighushi cheti kingine cha Sekondari namba 0217951 chenye indexi namba S 0310-0532,akionyesha ni halali na kwamba vimetolewa na Baraza la Mitihani Tanzania wakati akijua kuwa ni uongo.

Washtakiwa hao wamekana mashtaka na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi bado haujakamilika na washtakiwa kupelekwa rumande hadi Septemba 28, 2015 itakapotajwa.