May 21, 2015

SERIKALI YAOMBA RADHI KUCHELEWESHWA KWA MIKOPO VYUONI.NAIBU Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amewaomba radhi wanafunzi wote wa vyuo vikuu nchini, kwa kuchelewa kuwafikishia fedha zao za kujikimu. Hata hivyo, aLIsisitiza kuwa tangu juzi fedha hizozilishatoka Hazina.

Akizungumza bungeni jana alipokuwaakitoa majibu ya mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), Mwigulu aliagiza taasisi zinazohusika kuacha shughuli zote, ikiwemo vikao ili kuhakikisha fedha hizo zifike kwa wanafunzi hao jana.

Serikali imeshatoa fedha, naagiza taasisi zipeleke fedha hizo leo hii hii ili wanafunzi wasome tupate wataalamu wazuri, hii haitatokea tena,alisema Nchemba.

Awali, Bulaya aliomba Mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Lediana alipopewa nafasi, alisema wanafunzi 6,000 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamegoma kwa kuwa hawajapelekewa fedha hizo na hawana ugomvi na kitu kingine.

Kwa mujibu wa Bulaya, wanafunzi hao wanaipenda Serikali yao, lakini kuchelewa kwa fedha hizo, kumesababisha mateso kwa wanafunzi hao ambao wengi ni watoto wa masikini wanaotokea vijijini, huku wanafunzi wa kike wakiathirika zaidi.Bulaya alisema hata jana alipokuwa akizungumza bungeni, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph cha Dar es Salaam, kilikuwa kimefikia uamuzi wa kurejesha nyumbani wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza, kutokana na uchelewaji wa fedha hizo na kutaka Serikali ieleze kwa nini imechelewesha fedha hizo.

Akifafanua sababu ya kuchelewa kwafedha hizo baada ya kuomba radhi, Nchemba alisema Hazina iliamua kubadilisha utaratibu wa utoaji wa fedha kwenda maeneo mbalimbali.Alisema kwa utaratibu huo mpya, iliamuliwa kuwa fedha zinazotakiwa kwenda katika mifumo rasmi, ziwe zinapewa kipaumbele kwa kupelekwa kwanza kabla ya maeneo mengine ili uchelewaji wa fedha hizo usitokee tena.